Mbunge ataka kauli ‘magofu’ kutokuendelezwa ujenzi Dar

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:47 AM Apr 18 2024
Moja ya majengo ambayo hayajamaliziwa.
PICHA: MAKTABA
Moja ya majengo ambayo hayajamaliziwa.

MBUNGE wa Kinondoni (CCM), Tarimba Abbas, ameitaka serikali itoe kauli kuhusu majengo ambayo ujenzi wake umesimama kwa muda mrefu jijini Dar es Salaam pamoja na kuweka sheria ya ukomo wa ujenzi.

Hata hivyo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa rai watu ambao hawajakamilisha ujenzi wa majengo yao katika miji mbalimbali watumie utaratibu wa sera ya ubia ili kukamilisha ujenzi wa majengo hayo.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Geophrey Pinda amekiri kuwapo na baadhi ya majengo ambayo ujenzi umesimama kwa muda mrefu jijini humo na maeneo mengine nchini.

Amesema hali hiyo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na baadhi ya waendelezaji kujenga majengo kwa kutumia fedha zao binafsi za kudunduliza hali inayosababisha kuchukua muda mrefu.

“Katika kuwezesha upatikanaji mikopo ya nyumba nchini, Bunge lilitunga Sheria ya Mikopo ya Nyumba Na. 16 ya mwaka 2008, ili kuwezesha benki za biashara kutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa nyumba,” amesema.

Amefafanua kuwa mikopo katika benki hizo imekuwa na riba kubwa jambo ambalo linawafanya Watanzania wengi kushindwa kumudu mikopo hiyo pamoja na kusababisha gharama za nyumba zinazojengwa kuwa kubwa.

“Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa kunakuwepo mazingira wezeshi ya ujenzi wa majengo, ikiwa ni pamoja na kuhimiza ushindani katika sekta ya fedha ili kuwezesha kushuka kwa riba za mikopo ya nyumba mathalan kutoka asilimia 21 ya sasa hadi asilimia 12,” amesema.

Aidha, amesema serikali imekuwa ikihimiza uzingatiwaji wa sera ya ubia katika uendelezaji wa majengo mijini ili kuunganisha nguvu ya mitaji katika sekta binafsi na hivyo kuwezesha kukamilika kwa ujenzi wa majengo kwa wakati.