Majaliwa aagiza uwanja wa ndege Ibadakuli kutumika usiku

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 11:39 AM Feb 17 2025
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwaaga viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kukagua ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Ibadakuli Manispaa  ya Shinyanga, akitokea mkoani Simiyu.
Picha: Marco Maduhu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwaaga viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kukagua ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, akitokea mkoani Simiyu.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema anaridhishwa na viwango vya ujenzi wa uwanja wa ndege uliopo Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga, huku akimuagiza mkandarasi kufunga taa ili, uanze kutumika nyakati za usiku.

Majaliwa aliiagiza kampuni ya CHICCO, inayojenga uwanja huo, alipofanya ziara fupi ya kukagua upanuzi wa uwanja, Februari 16, 2025 alipowasili, kwa ajili ya kusafiri akitokea mkoani Simiyu.

Amesema serikali itaendelea kutekeleza miradi mingi ya kimkakati na kwamba katika upanuzi wa uwanja huo, wa ndege, hana wasiwasi na viwango vyake ya ujenzi, kutokana na mkandarasi huyo tayari ametekeleza miradi mingine yenye viwango.

“Uwanja huu wa ndege Ibadakuli hapa Shinyanga umeshakamilika kwa asilimia kubwa na miundombinu mingi ya muhimu imekamilika. Mimi nimeutumia kwa kutua na kuondoka, ila bado kuna mapungufu ya taa.

“Nakuangiza mkandarasi weka taa haraka, ili ndege zianze kutua usiku na siyo mchana tu, ili wananchi waanze kupata huduma ikiwamo na mikoa jirani,” amesema Majaliwa.

“Ndege za ATCL, serikali, zinasubiri ratiba tu kuanza kuutumia uwanja huu, TANROADS na msimamizi wa upanuzi ujenzi wa uwanja huu, msimamieni mkandarasi awekee taa haraka na mtumie jengo la zamani la abiria, wakati mkisubiri hili jipya kukamilika,” ameongeza.

Majaliwa aagiza uwanja wa ndege Ibadakuli kutumika usiku
Aidha,amesema dhamira ya serikali ni kurahisisha sekta ya usafiri, ukiwamo wa anga na kwamba karibu mikoa yote nchini, vinajengwa viwanja vya ndege kasoro ambayo ni mipya.

Ametoa wito pia kwa vijana ambao wamepata ajira kwenye ujenzi wa uwanja huo, kwamba wafanye kazi kwa weledi pamoja na kupata ujuzi, ili mradi huo utakapokamilika kujengwa na wao wafungue makampuni yao ya ujenzi.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwamba katika utawala wake ndani ya miaka minne, ameutendea haki mkoa huo.

Amesema miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa, huku akimuomba Waziri Mkuu, kufanya ziara ya kikazi mkoani humo, ombi ambalo alilikubali

Majaliwa aagiza uwanja wa ndege Ibadakuli kutumika usiku
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana,a Ajira na Watu Wenye Ulemavu, amepongeza Rais Samia kwa kugusa maisha ya wananchi wa Shinyanga na kwamba uwanja huo ulikuwa ni kilio cha muda mrefu, lakini sasa umeshaanza kutumika kwa hatua za awali.

Meneja Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Samweli Mwambungu, akitoa taarifa ya ujenzi wa uwanja huo wa ndege, amesema barabara ya kutua na kuruka ndege, imekamilika kwa asilimia 100, uzio (60), jengo la abiria (50) na linatarajiwa kukalimika Aprili Mosi, mwaka huu.

Amesema kwa upande wa fidia Sh. milioni 764 zimeshalipwa kwa wananchi ambao walikuwa jirani na uwanja huo, ili kupisha upanuzi, huku zikitolewa pia ajira 160, kati yao wazawa wakiwa ni 130 na kwamba mkandarasi ameshalipwa pesa zake zote na bado yupo ndani ya mkataba na gharama za ujenzi huo ni Sh. bilioni 49.