JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia madereva, John Peter (45), Mkazi wa Manyire wilayani Arumeru na Jafari Shirima (62), Mkazi wa Singida kwa tuhuma za kumsababishia kifo cha abiria, Lucy John (40), Mkazi wa Manyire.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Justine Masejo jana alisema kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kusababisha kifo cha abiria huyo, Februari 12, mwaka huu majira ya usiku eneo la Nganana Barabara ya Afrika Mashariki.
Masejo, alisema Peter akiendesha gari aina ya Toyota Noah, aliligonga kwa nyuma lori lilikokuwa likiendeshwa na Shirima na kusababisha kifo cha abiria huyo aliyekuwa kwenye gari lake.
Alisema kuwa baada ya kugonga lori hilo kwa nyuma, Peter anadaiwa kumshambulia Masawe kwa kitu chenye ncha kali na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
"Majeruhi anaendelea kupatiwa matibabu na mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalam,"alisema.
Masejo, alitoa wito kwa kwa madereva kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.
"Pia tunatoa wito kwa watu kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi yanapotokea matukio, kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED