Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), ametoa msaada wa kiti mwendo kwa Anjel Daniel (6), mtoto mwenye ulemavu mkazi wa Kitangili, Manispaa ya Shinyanga.
Msaada huo ulikabidhiwa jana kwa niaba ya mbunge huyo na Katibu wake, Samweli Jackson.
Akizungumza wakati wa makabidhiano, Samweli alisema Mbunge Katambi anaendelea kuguswa na changamoto za watu wenye uhitaji na mara zote amekuwa mstari wa mbele katika kuzitatua. Alieleza kuwa baada ya kupokea maombi kuhusu uhitaji wa kiti mwendo kwa mtoto huyo, Mbunge aliguswa na kuamua kutoa msaada huo kwa mama yake mzazi.
"Kwaniaba ya Mbunge Katambi, namkabidhi mama mzazi wa mtoto huyu kiti mwendo. Ameahidi kuendelea kumsaidia zaidi na anawaomba wazazi wenye watoto wenye ulemavu wasiwafiche ndani, kwani yupo kwa ajili yao. Hii pia ndiyo dhamira ya wizara anayofanyia kazi," alisema Samweli.
Kwa upande wake, mama mzazi wa mtoto huyo, Doricas Daudi Yacob, alimshukuru Mbunge Katambi kwa msaada huo na kumuomba aendelee na moyo huo wa kusaidia watu wenye uhitaji. Alisema amekuwa akimfuatilia kupitia vyombo vya habari na kuona jinsi anavyosaidia jamii.
Naye mdau wa maendeleo, Hashimu Issa, alieleza kuwa walimuona mama wa mtoto huyo akiomba msaada kupitia vyombo vya habari, jambo lililowagusa na kuamua kumsaidia pia kwa kumpatia dawa za matibabu ya mtoto wake. Aliwasiliana na Mbunge Katambi, ambaye sasa ameanza kutekeleza msaada huo kwa vitendo. Alimpongeza kwa namna anavyowajali watu wenye uhitaji na kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED