Jenerali Kahariri ateuliwa kumrithi Ogolla

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:44 PM May 02 2024
Luteni Jenerali Charles Muriu Kahariri awa Mkuu mpya wa Majeshi Kenya.
PICHA: MAKTABA
Luteni Jenerali Charles Muriu Kahariri awa Mkuu mpya wa Majeshi Kenya.

RAIS wa Kenya, William Ruto ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini humo, amempandisha cheo Luteni Jenerali Charles Muriu Kahariri na kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) wa Kenya.

Uteuzi huo wa Jenerali Kahariri unakuja Wiki mbili baada ya Jenerali Francis Ogolla kufariki dunia katika ajali ya helikopta pamoja na Maafisa wengine tisa wa kijeshi. 

Nafasi ya CDF hushikiliwa na Majenerali kutoka vikundi vitatu vya kijeshi ambavyo ni pamoja na Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Anga na Jeshi la Wanamaji la Kenya ambapo Jenerali Ogolla alikuwa anatoka kwenye Jeshi la Anga la Kenya huku Kahariri akitoka Jeshi la Wanamaji la Kenya. 

Rais Ruto pia amempandisha cheo Meja Jenerali John Mugaravai Ornenda hadi cheo cha Luteni Jenerali hadi kuwa Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Luteni Jenerali John Mugaravai Ornenda alikuwa Kamanda wa Jeshi la Wanahewa la Kenya kabla ya uteuzi huo. 

Rais Ruto pia amemteua Meja Jenerali Fatuma Gaiti Ahmed kwa Jeshi la Wanahewa la Kenya na Kamanda wake na pia amemteua Meja Jenerali Paul Owuor Otieno kwa Jeshi la Wanamaji la Kenya na kumteua kuwa Kamanda.