Katika hatua inayolenga kubadili taswira ya utalii wa Tanzania, Kampuni ya Maendeleo Hospitality Ventures (MHV), inayoongozwa na wawekezaji wa Kimarekani, imetangaza mpango wa kujenga hoteli ya kifahari yenye hadhi ya nyota tano katika Kijiji cha Robanda, karibu na Lango la Fort Ikoma la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mpango huo unalenga kuimarisha hadhi ya Tanzania kama moja ya maeneo bora ya utalii duniani, huku ukiwahamasisha ukuaji wa uchumi wa eneo husika na kuongeza fursa za ajira kwa jamii inayozunguka hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya MHV iliyotolewa leo, hoteli hiyo itakuwa mfano wa huduma za kimataifa, ikiwapa wageni fursa ya kipekee ya kutazama wanyamapori kwa mtazamo wa kuvutia zaidi na kufurahia uzuri wa asili wa Serengeti.
Mwenyekiti wa MHV, Rishen Patel, alieleza furaha yake kuhusu mradi huo, akisema: "Maono yetu ni kubadilisha huduma za hoteli nchini Tanzania kwa kuanzisha hoteli za kifahari zinazosherehekea urithi wa kiutamaduni na mandhari ya kipekee. Serengeti, inayojulikana kwa Uhamaji Mkubwa wa Wanyama, ni mahali sahihi kwa mwanzo wa safari yetu.”
Patel alisisitiza kuwa sekta ya utalii nchini Tanzania imekua kwa kasi katika muongo uliopita, huku idadi ya watalii ikifikia milioni 1.8 mwaka 2023 na kuingiza mapato ya Dola za Kimarekani bilioni 3.37. Takwimu za Agosti 2024 zinaonyesha ongezeko kubwa la watalii wa kimataifa hadi zaidi ya milioni 2, huku mchango wa sekta hiyo kwa uchumi ukitarajiwa kufikia Dola bilioni 3.5.
"Mwelekeo huu unaonesha maslahi makubwa ya kimataifa kwa Tanzania kama kituo maarufu cha utalii, pamoja na juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu na kuendeleza utalii endelevu,” alibainisha Patel.
Kwa upande wa uwekezaji, Patel alithibitisha kuwa MHV imeshirikiana na kampuni ya CORE Securities Limited ili kuwezesha upatikanaji wa mtaji kupitia Ofa ya Umma (IPO). Mpango huo unahusisha kuorodhesha asilimia 31 ya hisa kwa wawekezaji wa Kitanzania, huku asilimia 3 ikitengwa kwa jamii za eneo la mradi na asilimia 2 kwa wafanyakazi wa hoteli hiyo.
"Tunaamini huu ni wakati sahihi wa kuzindua mradi huu wa kipekee wenye ushirikishwaji wa Watanzania. Hoteli yetu ya Serengeti ni mwanzo tu, tunatarajia kuanzisha miradi mingine Zanzibar, Ngorongoro, na Kilimanjaro kwa lengo la kuvutia wageni kutoka kote ulimwenguni," alisema Patel.
Afisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka, alithibitisha kuwa kampuni yake inaendelea kuratibu uzinduzi wa IPO hiyo, akisema:
"Tunajivunia kuwa sehemu ya mradi huu wa kimataifa. Uwekezaji huu si tu kwamba utaongeza fursa za ajira, bali pia utatoa nafasi kwa Watanzania kumiliki sehemu ya hoteli hii kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam."
Fumbuka aliongeza kuwa hatua za mwisho za mazungumzo na mamlaka husika zinaendelea, huku lengo likiwa kuzindua Ofa hiyo kwa Umma ndani ya mwezi mmoja na hoteli hiyo kufunguliwa rasmi ifikapo Julai 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED