Watangaziwa fursa soko la hewa ya ukaa

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 08:04 AM Jan 23 2025
Hewa ya ukaa.
Picha: Mtandao
Hewa ya ukaa.

WAKAZI mkoani hapa wamehamasishwa kuchangamkia fursa ya kupanda miti kwa wingi ili kufikia soko la kimataifa la uvunaji wa hewa ukaa na kukuza uchumi wao.

Wito huo ulitolewa juzi na Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Maxon Msigala wakati wa kampeni ya upandaji miti katika eneo oevu la Lunyanywi ili kukabiliana mabadiliko ya tabia ya nchi lililoratibiwa na Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Mkoa wa Njombe.

Msigala, alisema kwa sasa hewa ya ukaa ipo sokoni, hivyo wananchi wakipanda miti ya kutosha na kuuza kwa kampuni za baadhi ya mataifa duniani ikiwemo Marekani.

“Kwa maana wanaangalia kiwango cha mti kilichopo na wanathaminisha na kiwango cha hewa ya ukaa kinachopatikana pale, hivyo mnakuwa mnalipwa fedha,” alisema Msigala.

Alisema fursa hiyo inaweza kuwa na uwezo wa kubadilisha hali ya uchumi kwa mkulima mjini Njombe.

“Nawahimiza kushiriki kwa wingi ili kuhakikisha mnakumbatia maendeleo yanayoendana na mahitaji ya dunia kwa sasa,” alisema Msigala.

Kwa upande wao wanachama hao, akiwemo Esther Mtanga alisema kwa kushirikina na maofisa wa maliasili wamepanda miti zaidi ya 100 ikiwa ni kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuteuliwa kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katibu wa Chama hicho, Saada Msangi, alisema wanatuma salamu za pongezi kwa Rais Samia kwa kupanda miti ili kumuunga mkono kwenye mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.

 Fursa ya kupanda miti kwa ajili ya soko la hewa ukaa ni hatua muhimu ya kiuchumi na kimazingira katika mkoa wa Njombe.