Pasaka iwe chachu ili kuleta mabadiliko kwa Watanzania

Nipashe Jumapili
Published at 11:05 AM Apr 09 2024
Kanisa.
PICHA: WINGU LA MASHAHIDI
Kanisa.

LEO ni Pasaka. Wakristo nchini wanaungana na wenzao duniani kote kukumbuka kufufuka kwa Mwokozi wao, Yesu Kristo, yapata miaka 2,000 iliyopita. Sikukuu hii inaadhimishwa ikiwa ni siku ya tatu, kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu, baada ya kuteswa, kuangikwa msalabani na hatimaye kufa na kuzikwa.

Sikukuu hii inasherehekewa baada ya juzi kuadhimisha Ijumaa Kuu, ikiwa ni kumbukumbu ya kuteswa hadi kufa kwa Mwokozi wao, huhanikizwa na ibada mbalimbali katika makanisa na madhehebu mbalimbali, huku maaskofu, wachungaji na mapadri wakitoa ujumbe mbalimbali kupitia mahubiri yao unaohusu maisha ya Ukristo na yale ya kawaida. Pia viongozi wa serikali hutoa salamu na ujumbe katika ibada zile za kitaifa na za kawaida. 

Wakristo, hasa wale ambao hufuata imani sawasawa, wanasherehekea Pasaka ikiwa pia ni kumalizika kwa mfungo wa Kwaresma. Waumini hao hufunga siku 40 kama alivyofanya Yesu Kristo na hatimaye akajaribiwa na shetani. 

Mbali na Pasaka kuadhimishwa kwa ibada, nchini Tanzania Wakristo huungana pia na watu wa imani zingine katika kusherehekea kwa kula na kunywa kutokana na mizizi ya kihistoria iliyojengwa kuonyesha kuwa wananchi ni wamoja na wanashirikiana katika masuala mbalimbali bila kujali imani, asili, kabila wala itikadi zao. Ndiyo maana licha ya ibada, katika kusherehekea Sikukuu za Kikristo na zile za Kiislamu, watu hujumuika pamoja katika kula na kunywa. 

Kama ilivyo ada, baada ya kufanyika kwa ibada, watu watajumuika majumbani na kwenye maeneo ya burudani kwa ajili ya kubadilishana mawazo, kula na kunywa. 

Pamoja na kwamba ni sikukuu kubwa kwa Wakristo katika kukumbuka maisha ya Yesu Kristo na kwamba ni ushindi kwao kutokana na kufufuka kwake, baadhi ya watu huigeuza kuwa siku ya kuyageukia mambo ya zamani waliyokuwa wakiyafanya kabla ya Kwaresma. 

Katika kipindi cha Kwaresma, baadhi ya watu hufunga na wengine kujizuia kufanya matendo ambayo ni kinyume cha maisha halisi ya Ukristo lakini inapofika siku kama ya leo, huyageukia mambo yale na kufanya maasi. Watu hao hulewa kupitiliza na wengine kuendelea kufanya uasherati na hata ushirikina. Kwa maneno mengine, watu hao hula matapishi yao.

Kwa ujumla, Pasaka ina maana pana kwa maana ni zaidi ya kushangilia kufufuka kwa Yesu Kristo ambaye kwa imani ya Kikristo, Mwenyezi Mungu alimleta duniani kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu kutoka katika maisha ya dhambi na kuwapatanisha naye baada ya uasi uliofanywa na Adam na Hawa na hatimaye kufarakana na Mungu. 

Kutokana na imani hiyo na kwamba Yesu Kristo amefufuka, hivyo waamini wamepata ushindi, ni vyema watu wakayaendeleza mambo mazuri waliyokuwa wakiyafanya katika kipindi ha mfungo wa Kwaresma kwa kutenda mema na kujizuia kutenda baadhi ya mambo ambayo ni chukizo mbele za Mungu. Wakristo hawana budi kuamini kwamba kwa kufa na kufufuka kwake, ameshinda dhambi na wako huru dhidi ya mambo yote ambayo hufanywa katika giza na uovu. 

Mwanafalsafa na Kiongozi wa zamani wa India, Mahatma Gandhi, aliwahi kusema: “Iwapo Wakristo wangeishi maisha kama aliyoyaishi Yesu Kristo, dunia ingekuwa na amani.” Lakini kutokana na watu hao na wengine duniani kuishi maisha yaliyo kinyume na Yesu Kristo, dunia imejaa machafuko, maasi na mabaya ya kila aina, hivyo amani na upendano vimetoweka.

Hayo yote yamesababisha kuwapo kwa mapigano baina ya taifa na taifa, kabila na kabila, watu kukosa hofu ya Mungu, wenye nacho kuwanyanyasa wasio nacho, walioko madarakani kutumia nafasi zao kujinufaisha badala ya kuwajali wananchi. 

Wakati leo Wakristo duniani kote wanaadhimisha siku hii ya kipekee ya Pasaka, wanapaswa kurejea misingi ya imani hiyo kwa kuyaacha mambo yasiyo faa na kutenda mambo na kuishi maisha kama aliyoyaishi Yesu Kristo alipokuwa duniani. 

Ni imani kwamba waumini hao kama watafanya mambo yenye ushuhuda mwema na kujiepusha na tamaa na kufanya yaliyo chukizo mbele za Mwenyezi Mungu na wanadamu, hakika kutakuwa na mabadiliko chanya na Tanzania itakuwa kielelezo cha watu Afrika na dunia nzima.