Kwa mambo haya aliyoyafanya Karume ataendelea kuenziwa

Nipashe Jumapili
Published at 06:12 PM Apr 07 2024
Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume.
PICHA: MAKTABA
Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume.

LEO ni kumbukumbu ya miaka 52 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aliyeuawa Aprili 7, 1972. Watanzania wanamkumbuka kiongozi huyo kwa mambo mengi aliyoyafanya kwa ajili ya Wazanzibari kwa kujitoa kwake kwa ajili ya ustawi wao.

Karume kwa kushirikiana na Wazanzibari wenzake, akiwamo Tito Okello, Ramadhani Haji Faki na Abdallah Said Natepe, walijitoa muhanga kuikomboa Zanzibar kwa kuongoza Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 yaliyomng’oa Sultani visiwani humo. 

Baada ya Mapinduzi hayo, Karume alitangaza kuwa Wazanzibari wote ni sawa bila kujali imani, rangi wala asili zao. Kutokana na hilo, alisema Mwafrika anaweza kumwoa Mwarabu na mhindi akamwoa Mwafrika au vinginevyo. Yote hiyo ni kuonyesha kuwa hakuna ubaguzi wa rangi miongoni mwa watu wa Zanzibar.

Jambo kubwa lingine aliloliweka hadharani  ni usawa katika umiliki wa ardhi na maisha bora kwa wananchi wote. Alitangaza ardhi kuwa chini ya serikali na wananchi wote watapewa sehemu ili waitumie kwa ajili ya uzalishaji mali.

Sambamba na ardhi, alifanya kwa vitendo kuhakikisha wananchi wanakuwa na makazi bora kwa kujenga maghorofa, maarufu kama nyumba za maendeleo Michenzani, Unguja na kisiwani Pemba. Majengo hayo yaliwanufaisha wengi na hiyo ilionyesha kuwa kiongozi huyo alikuwa na dhamira ya dhati katika kuleta ustawi wa watu wa visiwa hivyo. 

Karume pia hakupenda makuu wala madaraka makubwa na hiyo ilijidhihirisha mwaka 1964 alipokutana na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na kukubaliana kuziunganisha nchi zao na kuwa na taifa moja. Karume alikubali na kujishusha kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania huku akimwachia Nyerere kuwa Rais. 

Kiongozi na mwanamapinduzi huyo hayuko duniani zaidi ya nusu karne sasa lakini matendo yake na mema aliyoyafanya kwa ajili ya taifa yanamfanya aendelee kukumbukwa. Kwa matendo yake, Karume alijenga upendo na umoja wa kitaifa, misingi bora ya kiuchumi, kuleta haki na kupambana na dhuluma dhidi ya wanyonge.

Baada ya kufariki dunia, mambo mengi aliyokuwa akiyahimiza, ambayo yalikuwa njozi zake za juu ya Zanzibar anayoitaka kwa ustawi wa wananchi, yako mambo mengi ambayo yametekelezwa na yanaendelea kufanywa viongozi waliofuata baada yake. Mambo hayo yote yanaonekana katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, ardhi na makazi bora, kubwa zaidi, ni maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Moja ya falsafa ya Mzee Karume ambayo inaendelezwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya sasa, chini ya Rais Dk. Hussein Mwinyi, ni sera ya uchumi wa buluu ambayo inaakisi ndoto za Karume na waasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa manufaa ya Wazanzibari na watu wote duniani.

Kutokana na mazuri aliyoyafanya, kila inapokaribia kumbukizi yake, makongamano mbalimbali yamekuwa yakiandaliwa ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wake huku mambo mbalimbali yakisisitizwa ikiwamo kujenga tabia ya uzalendo wa kuipenda nchi na maendeleo ambayo ni falsafa ya kiongozi huyo.

Wakati wa kongamano la mwaka huu lililoandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere katika Kampasi ya Karume, Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi, alisema fikra na falsafa za kimaendeleo na kizalendo za Mzee Karume hazina budi kuendelea kuenziwa kwa maslahi ya taifa.

Dk. Mwinyi aliweka bayana kuwa Mzee Karume alijenga upendo na umoja wa kitaifa, misingi bora ya kiuchumi, kuleta haki na kupambana na dhuluma dhidi ya wanyonge, hivyo Watanzania hawana budi kumuenzi kwa vitendo. Pia aliwasisitiza Watanzania kujikumbusha misingi ya utendaji wenye kuacha alama katika maisha kwa kuendeleza na kukuza uzalendo.

Kwa mambo aliyoyafanya ikiwamo kujitoa muhanga kwa ajili ya taifa bila kujali maslahi binafsi, Watanzania wanapaswa kumuenzi Mzee Karume. Viongozi  kwa upande wao, wanapaswa kuiga nyayo zake kwa kujali maslahi ya wananchi.