Mbunge Maige: Rais Dk.Samia ametutendea haki Tabora Kaskazini

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 02:35 PM Apr 07 2024
Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini-Uyui mkoani Tabora.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini-Uyui mkoani Tabora.

Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini-Uyui mkoani Tabora, Almas Maige amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha miradi mingi ya maendeleo jimboni humo kwa ustawi bora wa wananchi.

Ametoa pongezi hizo juzi wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa Fedha 2024/2025 bungeni jijini Dodoma.

"Kwanza nianze na shukurani, Mheshimiwa Spika, Jimbo la Tabora Kaskazini, Mama Samia Suluhu Hassan kalitendea haki sana, kwa hiyo ninamshukuru sana na tunampongeza sana."

Mheshimiwa Maige amesema, ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika jimbo hilo miradi ya maendeleo ni mingi.

"Tumejenga majengo ya halmashauri ambayo hayakuwepo na ukumbi wa mikutano, lakini pia tumejenga hospitali ya wilaya.

"Lakini, vile vile tumejenga vituo vya afya vitatu, tumejenga shule mbili za sekondari, tumejenga shule moja mpya ya msingi, lakini vile vile tumekarabati madarasa, lakini pia tuna maji ya Ziwa Victoria vijiji 58 vya Tabora Kaskazini. 

"Tuna umeme vijiji vyote vya Tabora Kaskazini, tumejengewa barabara, tunajenga kituo cha VETA na bado tunapata elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita.

"Mheshimiwa Spika, mambo haya si madogo kwa jimbo moja ambalo limepata jumla ya shilingi bilioni 55.6 katika kipindi cha miaka mitatu.

"Tunamshukuru sana Mama Samia, tunampongeza sana Mama Samia tumeona kwamba Mama huyu ni mwenye utu, upendo na ulezi kwa jimbo letu la Tabora Kaskazini,"amefafanua Maige.