Wapatiwa elimu usalama watalii

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:04 AM Jun 09 2024
Wanafunzi toka Chuo cha Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi kutoka mkoani Mwanza wakiwa Katika kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia Jijini Arusha kwa ajili ya kujifunza namna ambavyo Kituo hicho kinafanya kazi ya kuwahudumia Watalii.
Picha: Polisi Arusha
Wanafunzi toka Chuo cha Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi kutoka mkoani Mwanza wakiwa Katika kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia Jijini Arusha kwa ajili ya kujifunza namna ambavyo Kituo hicho kinafanya kazi ya kuwahudumia Watalii.

WANAFUNZI wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi mkoani Mwanza, wamefika katika kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia jijini Arusha kwa ajili ya kujifunza namna kituo hicho kinafanya kazi ya kuwahudumia watalii na wageni wanaofika mkoani hapa.

Mkuu wa Kituo hicho, Mrakibu (SP) Waziri Tenga, alibainisha juzi kuwa wanafunzi hao wamepata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kuzingatia usalama wa watalii na wageni pindi wanapowahudumia.

Aidha, SP Tenga aliwasihi wanafunzi hao kuhakikisha wanakwenda kutoa huduma bora kwa watalii kwa sababu wageni wengi huwa wanatarajia kuona wanapata huduma bora pindi wanapofika nchini. 

Tenga aliwaeleza wanafunzi hao namna ambavyo kituo hicho kimeimarisha uhusiano mzuri kwa kushirikiana na taasisi zingine za sheria na za kimataifa lakini pia kampuni zote za utalii ili kufikia lengo la serikali kuhusu usalama kwa watalii wakati wote.

Mkufunzi kutoka chuo hicho,  Grace Mahendeka, alsiema lengo la kuwaleta wanafunzi hao katika kituo hicho ni kupata uzoefu wa namna gani kesi mbalimbali za utalii zinashughulikiwa katika kituo hicho lakini pia kuimarisha mahusiano baina ya taaisisi hiyo na Jeshi la Polisi.

Naye Victor Christian,  mwanafunzi toka katika chuo hicho, alisema wamejifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja uhusiano mzuri baina ya polisi na kampuni za utalii na taaisisi zingine na kupata fursa ya kuona  zinaendeshwa katika kituo hicho.

Aidha, alibainisha kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuwa na uhusiano mzuri baina yao na taasisi mbalimbali likiwamo Jeshi la Polisi ili kuhakikisha watalii wanakuwa salama.