Maonesho ya kibiashara yawe chachu kuleta wawekezaji

Nipashe
Published at 09:48 AM Jul 04 2024
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi.
Picha:Ikulu
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi.

JANA Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho ya Kimataifa ya Biashara (DITF), yanayofanyika jijini Dar es Salaam, Barabara ya Kilwa, wilayani Temeke.

Maonesho hayo ya 43 ni maarufu Sabasaba na hushirikisha taasisi, mashirika, wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali.

Mbali na washiriki kutoka ndani ya nchi, vile vile huvutia wafanyabiashara wa nje ya nchi ambao huja kuonyesha bidhaa zao na kutafuta biashara.

Maonesho hayo yaliyoanza Juni 28, yanatarajiwa kukamilika Julai 13 na yanafanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.

Mwaka huu washiriki walitarajiwa kuwa 3,846. Maonyesho hayo yanatarajiwa kutengeneza ajira za muda 11,712 na kwa mwaka jana kulikuwa na washiriki 3,500  wa ndani walikuwa 3,233,  wa nje 267, nchi za nje 19, watembeleaji 300,701 na ajira za muda 11,687.

Nchi 26 zilizothibitisha kushiriki katika maonesho hayo Korea, Uturuki, India, Japan, Singapore, Syria, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Msumbiji, Indonesia, Mauritius, Oman, Misri, Iran, Pakistan, Rwanda na Comoro.

Nchi zingine ni Zambia, Ethiopia, Kongo DRC, Ghana, China, Urusi, Italia, Uganda, Kenya na Zimbabwe na nchi nyingi kati ya hizo zinakuja kuonesha teknolojia mpya za mashine mbalimbali.

Teknolojia hizo ni zile zinazohitajika na Watanzania katika kuanzisha viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, hivyo wafanyabiashara wa ndani ni fursa kubwa ya kutumia kujifunza kwa ajili ya kuongeza uzalishaji, ubora wa bidhaa pamoja na kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao.

Maonesho hayo yatakuwa na mambo mbalimbali yakiwamo ya siku maalum za nchi saba zinazoshiriki kwenye maonesho hayo, ambazo ni China, Japan, Korea, Iran, Misri, Urusi na India na kutakuwa na programu ya Sabasaba urithi wetu.

Kutakuwa na programu za mikutano ya ana kwa ana, siku za kampuni zinazojumuisha sekta mbalimbali ambazo zimeandaliwa kwa kushirikiana baina ya sekta binafsi na umma zikiwamo TIC, ZIPA, TPSF, CTI, TCCIA na ZNCC.

Lengo la siku hizo ni kuwawezesha wafanyabiashara wa kitanzania kupata fursa ya masoko ya nje.

Watanzania wote vikiwamo vikundi vya ujasiriamali, kampuni, taasisi za umma na binafsi ni fursa yao kushiriki kwenye maonesho hayo kwa kuwa ni jukwaa muhimu la kukutana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza teknolojia mbalimbali.

Kupitia maonesho hayo washiriki watapata maarifa ya kisasa ya uzalishaji, ufungashaji na usambazaji wa bidhaa, kupata masoko ya ndani na nje pamoja na ajira.

Maonesho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Tanzania: Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji’.

 Kaulimbiu hiyo inalenga kuonesha dunia kuwa serikali iko tayari na inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara na kuwekeza katika sekta mbalimbali za uzalishaji ikiwamo sekta ya viwanda, kilimo, teknolojia, uwekezaji na utalii.

Maonesho hayo yatumike kutangaza bidhaa za ndani ili ziweze kupata soko la nje. Pia ni wakati wa kutumia teknolojia ya kisasa kuuza bidhaa zetu.