LICHA YA ZUIO LA BoT: Mikopo umiza mtandaoni yashika kasi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:41 AM Nov 26 2024
LICHA YA ZUIO LA BoT: Mikopo umiza mtandaoni yashika kasi
Picha: Mtandao
LICHA YA ZUIO LA BoT: Mikopo umiza mtandaoni yashika kasi

SIKU tano baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutangaza orodha ya programu tumizi (applications) 69 ambazo haziruhusiwi kutoa huduma ya mikopo mtandano, baadhi zimeendelea kutoa huduma hiyo huku matangazo yake yaliyodhaminiwa katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram yakishika kasi.

Hivi sasa kila aliyepakua programu tumizi ya mkopo, anakutana na matangazo katika mitandao ya kijamii yakihamasisha kuchukua mkopo, wakijinasibu kuwa "masharti yao ni rahisi na unapatikana kwa muda mfupi".

Mwandishi amebaini matangazo hayo yamelipiwa ili yasambazwe kwa kila anayeweka taarifa au kutembelea mtandao wa kijamii na ambaye alipakua programu tumizi yoyote ya mkopo.

Vilevile, mwandishi wa habari hii ametembelea programu tumizi mojawapo na kuomba mkopo ambapo alipewa maelekezo ya kurejesha fedha hizo kwa lipa namba, ilhali programu hiyo ni miongoni mwa 69 zilizotangazwa kutotambuliwa na BoT siku tano zilizopita.

"Taarifa za akaunti zetu: Tafadhali kumbuka zifuatazo ni akaunti zetu rasmi za malipo. Ili kulinda usalama wa fedha zako, tafadhali tumia akaunti rasmi kwa ajili ya malipo. Airtel 540540; Vodacom 500555; Tigo 500555; na HaloPesa 500555."

Matangazo hayo mengi yanaeleza riba ya mkopo ni asilimia moja, muda wa mkopo ni siku 180 na kiasi ambacho mtu anaweza kukopa ni Sh. 500,000 hadi milioni moja, na hawaangalii historia ya mkopo.

Pia wanaeleza kwa picha mjongeo ambazo wasichana na wavulana wanatumika kueleza namna walivyojipatia mikopo, wakishawishi kuwa wamepata mikopo yao ndani ya dakika tatu tu. Kila tangazo wameambatanisha na link ya kubonyeza ili kupakua programu tumizi husika.

Jana mwandishi alitembelea programu tumizi kadhaa na kubaini bado wanahitaji taarifa binafsi za mkopaji, ikiwamo kuona picha zake kwenye kifaa chake, kuona namba za simu alizohifadhi, kuona ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) na kwamba bila kukubali masharti husika, hawezi kupewa mkopo.

"Hakuna uchaguzi wa kitambulisho, hakuna dhamana inayohitajika, hakuna ukaguzi wa mkopo. Unaweza kukopa hadi TZS 1,000,000 kwa dakika tatu tu," ilielezwa katika moja ya matangazo hayo.

Katika moja ya matangazo, mwananchi mmoja aliweka ujumbe aliotumiwa baada ya kuchukua mkopo na muda wa kulipa haujafika. Unasomeka:

"Ukiwa kama mtu mzima mwenye meno 32 na akili timamu, sijaona sababu ya wewe kukaa kimya mpaka sasa na kuzima simu ikiwa pesa zetu ulizifuata mwenyewe kwa dhiki ulizonazo na hakuna aliyekuita na uliona kuwa leo umepitiliza muda na bado unakaza mishipa ya fahamu, hutaki kulipa.

"Sasa una saa moja ya kukamilisha malipo yako ya ZIMACASH kabla kila mtu kwenye simu yako hajaanza kupata ujumbe wa udhalilishaji kutoka kwetu na kila mtu atajua kuwa umekopa ZIMACASH, jipange!"

Mwandishi wa habari hizi alifanya uchunguzi wa miezi minne na kubaini wakopeshaji wasiofuata utaratibu na wasiotambuliwa na BoT, huwadhalilisha na kuingilia taarifa binafsi za wakopaji.

BoT ilitoa mwongozo wa wakopeshaji mtandaoni, ikiwapa siku 14 kuwasilisha maombi yao, lakini kati ya waombaji 16 waliojitokeza ni wanne pekee waliokidhi vigezo hadi Novemba 21 mwaka huu taasisi hiyo ilipotoa orodha ya wakopaji wasiotambuliwa na kuitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzifunga programu tumizi wanazofungua.

PDPC YAONYA

Tume ya Ulinzi wa Taarifa binafsi (PDPC) imewaonya wakopeshaji dhidi ya matumizi ya taarifa binafsi. 

Jana, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk. Emmanuel Mkilia, alionya taasisi za mikopo zinazotoa taarifa za watu mitandaoni, akizitaka kuacha tabia hiyo mara moja, kwa kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Vilevile, alisema kuwa hadi kufikia mwezi huu, zaidi ya taasisi 700 za ukusanyaji na uchakataji taarifa binafsi nchini zimesajiliwa na tume hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema taasisi za mikopo mitandaoni hazipaswi kutoa taarifa binafsi za waliokopa kwa kuwa hilo ni kosa kisheria na wakibainika watachukuliwa hatua kali.

"Tume inawaalika wananchi wote kutoa taarifa kuhusu watu au taasisi zinazotoa taarifa zao bila ridhaa yao kwa sababu kuna sheria ya kulinda faragha za watu," alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa tatizo la kuvuja kwa taarifa hizo binafsi limekuwa na madhara makubwa kwa jamii, ikiwamo kusababisha baadhi ya watu kujitoa uhai wao.

Mkurugenzi huyo alisema ipo Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na. 11 ya Mwaka 2022 na kanuni zake ambazo zilitungwa kwa lengo la kulinda faragha ya watu.

Alisema mazingira ya kidijitali yameleta mabadiliko makubwa katika maisha ya kila siku na kusababisha taarifa binafsi na faragha za watu kuvujishwa.

Alisema tume hiyo itaendesha warsha inayotarajiwa kufanyika Dar es Salaam kwa lengo la kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu ulinzi wa taarifa hizo binafsi.