BAADA ya kuanza mzunguko wa pili kwa ushindi mnono, Yanga Princess imetamba itaendelea kutoa 'dozi' katika kila mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL), watakayocheza.
Kauli hiyo imetolewa baada ya Yanga Princess kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Bunda Queens, katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam juzi.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, kiungo mshambuliaji wa Yanga Princess, Neema Kiniga, alisema wanawaomba mashabiki na wanachama wa timu hiyo kutarajia mazuri katika mzunguko wa lala salama.
Nyota huyo alisema kikosi chao sasa kimeimarika na wanaamini watapambana kusaka ushindi ili kufikia malengo yao.
"Nafanya kile ambacho kocha ananielekeza, mimi ninazingatia sana maelekezo yake ninapokuwa kwenye uwanja wa mazoezi, ninaamini tutaendelea kuwa na matokeo mazuri katika mzunguko huu wa pili," alisema Neema ambaye alifunga bao la kwanza.
Mabao mengine katika mechi hiyo yalifungwa na Eragash Tandesse, Agness Palangyo na Asha Ramadhan.
Mechi nyingine iliyochezwa juzi, JKT Queens ilipata ushindi wa mabao 4-0 wakati Ceasiaa Queens iligawana pointi na Fountain Princess baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED