BAADHI ya mashabiki wa Yanga kutoka mikoa mbalimbali nchini waliokuwa wamekuja jijini Dar es Salaam juzi kushuhudia mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini wameulalamikia uongozi wa klabu hiyo kwa kitendo cha kuruhusu mashabiki kuingia uwanjani bure hali iliyozua tafrani kubwa na kuwanyima nafasi ya kuishuhudia mechi hiyo mubashara uwanjani.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi na timu hizo kutoshana nguvu kwa sare tasa, uongozi uliruhusu mashabiki kuingia bure bila kulipa eneo lote la mzunguko ambalo ndilo linalochukua idadi kubwa zaidi ya watazamaji uwanjani hapo.
Kutokana na wingi wa mashabiki waliojitokeza na kila mmoja akitaka kuwahi nafasi, walivamia geti uwanjani hapo na kulivunja, hali iliyozua tafrani na wengine kuumia na kukimbizwa hospitali.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti baada ya mechi nje ya uwanja huo, baadhi mashabiki hao walisema kitendo hicho kimewasikitisha kwani wametumia gharama kubwa ya usafiri mpaka kufika Dar es Salaam, lakini wamelazimika kuangalia mchezo huo kwenye vibanda umiza na baa kutokana na kushindwa kuingia uwanjani.
Walisema kwa hicho kilichotokea viongozi wa Yanga wanapaswa kujifunza na kubadilika kwani mchezo mkubwa kama huo hawakupaswa kuruhusu mashabiki kuingia bure.
"Nimesikitika nimetoka Tunduma kuja hapa kuiangalia Yanga, nimekata tiketi mapema, lakini nimeambulia kuishia getini huu mchezo ni mkubwa ni bora wangeweka viingilio vya chini kila shabiki angelipa na kungekuwa na utaratibu mzuri kuliko hivi wanaweza kusababisha vifo vya watu wengi," alisema Kessy Hamisi.
Kessi alisema hajaridhishwa na uamuzi huo kutokana na gharama zake alizozitumia na kuwataka viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lifuatilie suala hilo vinginevyo ipo siku litaleta adhari kubwa.
Naye Zaituni Athumani kutoka Arusha, amewataka viongozi hao kutambua umuhimu wa timu kupata mapato kupitia mechi kubwa kama hiyo kwani nchi zilizoendelea huwezi kukuta kiingilio ni bure.
"Vya bure vinaua ndicho kilichotokea leo( juzi), uwanja umezidiwa watu ni wengi mno binafsi nimelaani vikali kitendo hiki kwa kuwa malengo yangu hayajatimia, kwani sikuiona mechi," alisema Zaituni.
Karim Khamis kutoka Dodoma alisema: "Unapotanga mechi kubwa kama hii bure kwanza tunaishusha thamani klabu yetu na mashabiki watakuwa wakisubiri vya bure kila wakati, hii haipendezi wengeweka hata buku mbili, nimetoka Dodoma nimeishia kuangalia mpira baa, si bora ningebaki nyumbani.
"Kwanza ukisema bure tu hata vibaka wanaongezeka, wengi nimesikia wakilalamika kuibiwa, ustarabu unakuwa mdogo hata walinzi maalum wanazidiwa ndio maana hata geti likavunjwa, hii ni hatari."
Moses John kutoka Moshi, Kilimanjaro alisema: "Hii si haki, kabisa, yani nimeteketeza hela yangu kutoka Moshi hadi hapa kuja kuangalia mechi kwenye TV Dar es Salaam.
"Ifike wakati tujifunze kwa wenzetu Simba, ambao wao wanajisikia fahari kulipa kiingilio kwenda kuisapoti timu yao licha ya msimu huu kutokuwa na matokeo mazuri kama misimu iliyopita, lakini wao wanajaza uwanja kwa kukata tiketi, ni aibu kwetu mpaka tusikie ni bure."
Juma Jafari wa Dar es Salaam, alisema alifika uwanjani mapema lakini tayari watu walikuwa wameshajaa uwanjani na kulikuwa hakuna sehemu ya kupita kutokana na wingi wa watu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED