Wanaswa kwa kughushi nyaraka wajipatie ardhi

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 04:45 PM Feb 18 2025
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, George Katabazi
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, George Katabazi

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma, limewakamata watu watano kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganjifu kiasi cha Sh. milioni 60, walizozipata baada ya kuuza kiwanja kwa kughushi nyaraka mbalimbali, ikiwamo hati za eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, alisema tukio hilo lilifanyika Januari 11, mwaka huu, saa 5:00 asubuhi maeneo ya Mlimwa C.

Alisema, watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya msako mkali, uliofanywa na jeshi hilo, tangu Februari 3 hadi Februari 16, mwaka huu.

“Watuhumiwa hawa ni Penina Mushi, mwenye umri wa miaka 34, mkazi wa Kilimahewa mkoani Mwanza na wenzake wanne wenye umri kati ya miaka 30 hadi 56, wote wakazi wa jiji la Mwanza,” alisema Kamanda Katabazi.

Alisema, watuhumiwa hao walighushi hati ya kiwanja hicho, chenye ukubwa wa mita za mraba 910, pamoja na nyaraka nyingine na kumwaminisha mnunuzi kuwa wana undugu wa karibu na mmliki wa eneo hilo na kujipatia kiasi hicho cha fedha.

“Baada ya kupata taarifa hizo jeshi la polisi liliendesha oparesheni maalum ya kusaka mtandao wa watuhumiwa hao a na kufanikiwa kuwatia nguvuni, uchunguzi bado unaendelea na ukikamilika watafikishwa pale wanapostahili,” alisisitiza Kamanda Katabazi.

Aidha, alisema oparesheni hiyo itakuwa endelevu, ili kuwakamta watu wote ambao wamekuwa wakijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kwa kutumia mahitaji  makubwa ya ardhi yaliyopo hivi sasa katika jiji la Dodoma.