MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ameutaka uongozi wa Kijiji Cha Gidabagara Kata ya Boay kuweka gharama rafiki kwa wakazi wanaotaka kuvuta maji majumbani ili kuwawezesha kupata huduma hiyo kiurahisi.
Kiongozi huyo ametoa agizo hilo mkoani huko alipokuwa akipozindua na kukabidhiwa mradi wa maji safi uliotekelezwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la Word Vision kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA).
Akizungumza baada ya kupokea mradi huo, Queen amesema malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kushirikiana na wadau binafsi sasa yanaonekana kwa vitendo.
"Maji ni uhai, leo nimekabidhiwa mradi wa msaada, mradi huu ni mkubwa sana hii kata ina vitongoji vitano, kwa ukubwa wa mradi utahudumia vitongoji vyote.
"Gharama zikiwa rafiki hawa wananchi wataingiza maji kwa wingi na sisi tutakusanya kile tunachotaka ninalishukuru sana Shirika la Word Vision kwa kazi kubwa waliyoifanya kufikisha maji Katika vitongoji vya Kijiji hiki" amesema Queen baada ya kuzindua na kukabidhiwa mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh Milioni 291.
Mkurugenzi wa Ubora na Mikakati wa Miradi Word Vision, Simon Moikani amesema mradi huo utanufaisha wanakijiji 2,498 na kwamba dhima kuu ni kuboresha ustawi wa maisha ya mtoto katika familia duni kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, inayojumuisha afya, usafi wa mazingira, maji, uchumi wa kaya, ufadhili, utetezi wa haki za watoto pamoja na elimu.
Amesema Word Vison kupitia mradi wake wa kuongeza uchumi wa kaya, imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika vijiji vya Sangara na Ayasanda ambao umewezesha wanavikundi 71 wanaolima mashamba yenye ukubwa wa hekari 198.
“Ni adhima ya World Vision kuona watoto na jamii za kitanzania wanaishi katika mazingira yenye uhakika wa upatikanaji wa maji safi na salama, na kuwaepusha Wanawake na adha ya kufuata maji umbali mrefu.
“Kadhalika, kupitia mradi huu shule ya Msingi Gidagabara yenye watoto wapatao 610 (wavulana 331 wasichana 279) tumeiwezeshwa kupata mabomba ya maji safi na salama ili kulinda afya za watoto wawapo shuleni” amesema Moikan
Mkazi wa Kijiji cha Gidagabara ulikokabidhiwa mradi wa maji Khadija Mmasi, amesemakabla ya mradi huo wa maji walikuwa wanapata shida sana na kwamba walikuwa wanalazimika kunywa maji ya kwenye bwawa ambayo hayakuwa salama kwa afya.
"Tunashukuru sana Word Vision kwa kutuletea huu mradi wa maji utatupunguzia adha tuliyokuwa tunapata awali, kilichobakia hapa ni kupambana tuvute maji nyumbani kwa sababu sasa tumesogezewa mpaka mdomoni.
"Ilikuwa shida sana wakati mwingine Mpaka watoto walikuwa wanachelewa shule, wanakosa vipindi vya masomo kwa sababu maji yalikuwa yanapatikana mbali lakini Sasa yapo jirani muda na saa yoyote ninaweza kuchota.
World Vision ni shirika la Kimataifa la Kikristo linalofanya kazi katika nchi mbalimbali duniani Kwa Tanzania, shirika hili lilianza kufanya kazi rasmi mwaka 1981.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED