WAKUU wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamemwidhinisha Rais William Ruto wa nchini Kenya kuwa Mwenyekiti Mpya wa jumuiya hiyo, baada ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, kumaliza muda wake.
Akizungumza baada ya kushika kijiti hicho, Rais Ruto alitaja vipaumbele sita atakavyovisimamia kipindi chake cha uongozi ikiwamo kuboresha maisha ya watu wa EAC.
Ruto alisema atahakikisha anaongeza ushindani wa kibiashara, kukuza uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa za ndani ya jumuiya hiyo.
Kipaumbele kingine alikitaja ni kuongeza imani miongoni mwa nchi wanachama na kuimarisha uwekezaji kwa faida ya uchumi EAC.
"Hivi ndivyo vipaumbele vyangu vya muhimu kwa ajili ya kuleta mageuzi ya uchumi wa EAC, kutengeneza ajira na kuhakikisha kuna maendeleo endelevu kwa nchini zote, amani, usalama na utulivu,"alisema.
Alisisitiza pia kusimamia suala la uwajibikaji wa kisiasa na utawala bora kwa kuwa ndiyo njia bora ya kuhakikisha uwapo wa utulivu endelevu katika jumuiya hiyo.
Alisema ili kufikia hayo, ni lazima EAC kuendelea kuimarisha mifumo ya kikanda ambayo inalinda mamlaka yao na usalama wa pamoja, huku akihimiza utawala jumuishi unaoakisi matarajio ya wananchi wa Afrika Mashariki.
"EAC ni Jumuiya yenye soko kubwa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu zaidi ya milioni 300 linalotoa fursa ya kujenga uchumi na kuimarisha biashara kwa manufaa ya watu wa EAC,"alisema.
Kuhusu lugha za Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa, Rais Ruto alisema zitaendelea kutumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku akisisitiza Kiswahili kubeba utamaduni wa watu wa Afrika na EAC.
Alimshukuru aliyempokea nafasi hiyo, Rais Kiir kwa uongozi wake wenye maono ulioiletea EAC mafanikio makubwa.
Awali, Rais Kiir kabla hajakabidhi uongozi kwa Rais Ruto, alisema suala la amani na usalama linapaswa kupewa kipaumbele .
Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Mkutano wa 24 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo uliofanyika jijini hapa, aliwataka wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujivunia Jumuiya hiyo kwa kuwa kuna mwanga mkubwa wa matumaini mbeleni.
Rais Samia aliwahakikishia wananchi wa EAC kuwa changomoto zozote zitakazoibuka hazitapewa nafasi ya kuwavunja moyo na kuwarudisha nyuma.
Alisema changamoto zinapoibuka baadhi ya watu hudhani ndiyo mwanzo wa jumuiya hiyo kusambaratika.
"Tunataka kuhakikishia watu wote tunakuwa wamoja na jumuiya moja, hivyo tunaposherehekea miaka 25, EAC inazidi kuimarika na kuelekea katika utangamano zaidi kama wimbo wetu wa EAC unavyosema, Kwa hiyo wananchi tujivunie jumuiya yetu," alisema.
Rais Samia alipongeza mafanikio yaliyofikiwa na EAC kwa miaka 25 ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya wanachama kutoka watatu mwaka 1999 hadi kufikia wanane sasa.
"Lakini ninakupongeza Rais Ruto kwa kuchukua nafasi ya Uenyekiti wa EAC na Rais Kiir aliyemaliza muda wake," alisema.
Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva alisoma takribani maazimio saba ya Wakuu wa Nchi za EAC ikiwamo kukiidhinisha Kiswahili kuwa moja ya Lugha rasmi za EAC baada ya Kiingereza na Kifaransa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED