KATIKA kuhakikisha wachezaji wake wanarejea haraka ili kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya mechi ya dabi, mabosi wa Yanga wameandaa utaratibu wa kuwarejesha mapema nyota waliokuwa kwenye timu za mataifa yao, imefahamika.
Mechi ya watani wa jadi ya mzunguko wa kwanza ambayo Simba watakuwa wenyeji itachezwa Oktoba 19, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, aliliambia gazeti hili jana, wameandaa utaratibu wa kuhakikisha wachezaji wao wote wanarudi nchini haraka na kwa njia rahisi, ili kujiepusha na uchovu wa kusafiri kwa muda mrefu ambao amedai huwa unawachosha wachezaji.
"Idara yetu ya utimamu kwa mwili imekuwa ikifanya mawasiliano na wachezaji wote kuhakikisha wanalinda miili yao na tunaangalia njia zote rahisi na nzuri kuhakikisha wanarudi mapema na salama, ili kuuwahi mchezo huo, wakiwa hawana uchovu.
Changamoto kubwa ambayo wachezaji wanaipata ni kusafiri, ukiangalia taratibu za kuunganisha safari za ndege kwenye jiografia ya bara la Afrika, mchezaji anatakiwa akae njiani kwa siku mbili, atoke nchi moja ya Afrika, aende mpaka Ulaya (Uturuki), akae saa 10 au 15 na pengine mpaka 20, halafu arejee tena Afrika, hii inafanya wachezaji kuwa na mchoko au fatiki, akifika badala ya kupumzika anatakiwa ajiandae na mchezo unaofuata wa klabu yake," alisema Kamwe.
Aliongeza hata makocha wanavyolalamika juu ya wachezaji wao kwenda kwenye vikosi vya timu za taifa, mara nyingi huwa ni usafiri na si kucheza mechi nyingi kwa muda mfupi.
"Waliopanga ratiba si watu ambao hawajui mpira, wapo sahihi kabisa, kila kitu kimepangwa ndani ya kanuni za soka na taratibu zake. Taratibu zinasema mchezaji anatakiwa kukaa saa 72 kabla ya kucheza mchezo mwingine, tatizo kubwa siku zote huwa ni usafiri tu, safari hii sisi tumeliangalia," Kamwe alisema.
Kuhusu mechi ya dabi, Kamwe alisema wameshazungumza na wachezaji wao, wanachohitaji ni kuzipata pointi tatu tu na si vinginevyo.
"Hakuna kombe la dunia pale, wala si fainali ya mashindano yoyote, ni mchezo wa Ligi Kuu tu, hata timu ipige visigino, kanzu, matobo au icheze mpira mzuri vipi, kinachotakiwa kwenye mchezo ule ni kuondoka na pointi tatu, kama hawatapata mashabiki hawatawaelewa, tumeshawaambia wachezaji wetu tunachohitaji ni ushindi wa mabao yoyote yale, hata ikiwa moja," aliongeza ofisa huyo.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga waliokuwa kwenye timu za taifa, ukiachilia mbali Watanzania ambao wao wanarudiana na DR Congo hapa nyumbani, watakaosafiri ni Clatous Chama na Kennedy Musonda waliokuwa kwenye kikosi cha Zambia ambayo ilienda kucheza dhidi ya Chad wakati Stephane Aziz Ki, akiwa na Burkina Faso iliyoishindilia Burundi mabao 4-1, na Djigui Diarra akiwa na Mali wao walikuwa wanakutana na Guinea Bissau nyumbani na ugenini.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi watashuka katika mechi hiyo wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi zao nne walizocheza na kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wako katika nafasi ya nne huku Simba yenye pointi 13, imeshinda michezo minne na kutoka sare moja.
Vigogo hao wawili wa soka nchini wote wametinga hatua ya makundi , Yanga ikishiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba yenyewe inapeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED