Mashindano ya Swalle Cup yameendelea kuwa kivutio kikubwa kwa vijana wa Mkoa wa Njombe na taifa na kupelekea kutajwa kuwa moja ya mashindano bora kwenye mkoa huo kwa kutoa vijana na kuwapeleka kwenda kufanya majaribio kwenye vilabu vikubwa nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa michuano hiyo uliofanyika katika Kata ya Mtwango inayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Lupembe Edwirn Swalle kwa awamu ya nne tangu ilipoanzishwa,mratibu wa michuano Hans Luwanja amesema ukubwa wa michuano hiyo umesadifu kulingana na fedha inayowekwa ambapo mpaka sasa kiasi cha shilingi Milioni 120 kimewekwa.
"Mashindano haya yamekuwa kivutio kwa wananjombe na taifa pia tunajivunia na kutembea vifua mbele kwani ni moja ya mashindano bora mkoani Njombe ni hii pia imetajwa kwa kugharamia kiasi cha shilingi Milioni thelathini kwa kila mwaka kwa miaka minne hivyo ni sawa na Milioni mia moja ishirini ambazo zitakuwa zimetumika," amesema Luwanja.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Lupembe Edwin Swalle amesema katika michuano ya mwaka 2024 wapo watu maalum walioingia ubia na watakaofika kwenye hatua ya nusu fainali kwa ajili ya kutafuta vipaji na kuwapeleka kwenye vilabu vikubwa huku akibainisha kuwa msimu wa mwaka 2023 Swalle Cup ilitoa matunda kwa kuwapeleka vijana kufanya majaribio katika Club ya Azam na mmoja wao amefanikiwa kupata mkataba wa kwenda kucheza mpira nchini Japan.
"Swalle Cup inaunga mkono kazi nzuri ya Rais wetu na tumemuona akitoa fedha kwa timu zinazofanya vizuri kwa hiyo Swalle Cup ya mwaka huu mshindi wa kwanza atapata Ng'ombe wa thamani ya zaidi ya Milioni 1.5, fedha taslimu shilingi laki tano, kombe la Swalle Cup lakini pia Jezi na Mpira wa ligi kuu na medali,"amesema Swalle.
Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Njombe Samwel Mgaya ambaye amesema jimbo la Lupembe limekuwa na umahili mkubwa hususani kwenye michezo ambapo ametoa wito vijana kuendelea kushiriki katika michezo ili kutimiza ndoto zao.
Kwa mwaka 2024 mashindano ya Swalle Cup yanakwenda kuhusisha timu za vijiji 45 zitakazo kuwa katika makundi mawili ikiwemo tarafa ya Lupembe pamoja na tarafa ya Makambako ambao watacheza jumla ya michezo yao ili kupata timu 12 mabingwa wa kata kwa ajili ya kumpata bingwa wa kata huku pia michuano hiyo ikitanuka zaidi kwa kuwa na ligi ya wanawake.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED