WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Washindi Afrika, Simba, leo saa 10:00 jioni watashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, wakiwa na dhamira moja tu ya kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya.
Simba inatarajia kukamilisha mipango yake hiyo leo baada ya Jumapili iliyopita kulazimisha suluhu ugenini dhidi ya timu hiyo iliyokuwa nyumbani, Uwanja wa Juni 11, jijini Tripoli.
Ni ushindi wowote ule ndiyo utaivusha Simba kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Mechi hiyo inayotarajiwa kuhudhiriwa na maelfu ya wanachama na mashabiki wa Simba, itashuhudiwa pia na mchezaji wa zamani wa AS Vita, Elie Mpanzu ambaye yupo nchini.
Winga huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo anayesemekana kuwa yupo nchini kwa ajili ya kumalizana na klabu ya Simba ili kujiunga kipindi cha dirisha dogo la usajili, atakuwepo jukwaani akiiangalia timu ambayo ilikuwa ajiunge nayo kipindi cha usajili mkubwa uliopita, lakini akapata ofa ya kwenda nchini Ubelgiji kufanya majaribio yaliyofeli katika klabu ya Klabu ya Genk.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema mchezo wa leo utakuwa tofauti na ule wa mwanzo waliocheza ugenini.
Alisema katika mchezo wa mwanzo, awali aliingia kuzuia na kushambulia kwa kushtukiza ili kusaka bao, lakini baada ya kuona wapinzani wao wanaingiza washambuliaji wengine, hasa kipindi cha pili, ndipo akaamua kupaki basi ili kuzuia wasipate bao.
"Hii ni tofauti na hapa, tutakachofanya ni kuzuia, lakini tutakwenda mbele kusaka mabao. Hatutaki wapinzani wetu waanze kupata bao kabla ya sisi kwa sababu utatuweka kwenye wakati mgumu na presha kubwa, tunachotaka ni kuwa na ukuta mgumu usiofungika, halafu ndiyo tunatafuta bao, tukilipata najua wataondoka nyuma kwa ajili ya kusaka bao la kusawazisha, hapo ndipo tutakapopata mwanya wa nafasi nyingi zaidi," alisema Fadlu raia wa Afrika Kusini.
Mechi ya leo imekuwa na presha kuwa hasa kwa wapinzani ambao wamekodisha mabaunsa wa kuwalinda wakihofia kulipiziwa kisasi kwa kile ambacho mashabiki wao walikifanya Jumapili iliyopita.
Mashabiki wa Al Ahli Tripoli, waliwafanyia fujo wachezaji na baadhi ya viongozi wa Simba, kabla, wakati wa mchezo na baada, kitu ambacho kiliifanya klabu hiyo kushtaki kwenye Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Hata hivyo, Rais wa CAF naye akiwa nchini Nairobi nchini Kenya, aliagiza uchunguzi ufanywe na hatua zichukuliwe kwa kile kilichotokea kwenye mchezo huo.
Kama itatinga makundi itakuwa ni mara ya pili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, kama ilivyofanya msimu wa 2021/22 na kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED