TIMU ya Soka ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, leo itafungua michuano ya kuwania Kombe la Afrika Mashariki kwa vijana chini ya umri huo, itakapokipiga dhidi ya Kenya, mechi ikichezwa, Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mchezo huo utafanyika saa 10:00 jioni, huku Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Charles Boniface Mkwasa, akisema kikosi chake kimejiandaa si kwa kushinda mchezo huo tu, bali kulibakisha kombe nyumbani.
"Nimeridhika na maendeleo ya kikosi changu, nadhani vijana wapo tayari, tutafanya vyema kwenye mashindano haya, hata kutwaa ubingwa," alisema Mkwasa.
Mbali na mchezo huo saa 10:00 jioni, majira ya saa 18:00 jioni kutakuwa na mchezo mwingine kati ya Sudan dhidi ya Djibouti, ambao utachezwa, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), michezo hiyo itaendelea tena kesho, Sudan Kusini itakapokipiga dhidi ya Burundi, Uwanja wa KMC Complex, saa 10:00 jioni na saa 12:00 jioni, Azam Complex, Uganda itakumbana na vijana wa Ethiopia.
Ratiba inaonyesha kuwa michuano hiyo itaendelea tena Jumanne, Tanzania, itakaposhuka kucheza dhidi ya Djibouti, Uwanja wa KMC Complex jioni, na Sudan kukipiga dhidi ya Rwanda, saa 12:00 jioni, Uwanja wa Azam Complex.
Michuano hiyo inayofanyika nchini mwaka huu, imegawanywa kwenye makundi mawili, A, likiwa na Tanzania, Rwanda, Sudan, Kenya na Djibouti, huku kundi B, likiwa na timu za Burundi, Ethiopia, Sudan Kusini na Uganda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED