KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, 'Taifa Stars', Hemed Suleman 'Moroco', amesema katika mchezo utakaochezwa Jumanne dhidi ya timu ya taifa ya Guinea, watashambulia zaidi tofauti na ilivyokuwa mchezo wa kwanza dhidi ya Ethiopia wa kufuz fainali za AFCON 2025.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kukwea pipa kuelekea nchini Ivory Coast ambako itachezwa mechi hiyo ya pili ya kusaka tiketi ya kucheza fainali hizo, Moroco alisema wamefanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokea kwenye mchezo uliopita.
"Huko tunakokwenda tunakwenda kushambulia, huo ndiyo mfumo tutakaotumia, kwa sababu hakuna kingine tena, tunahitaji pointi tatu.
Siamini sana nyumbani au ugenini, mpira siku hizi unachezwa popote pale, kwa jinsi tulivyocheza mechi iliyopita kipindi cha pili na tumerekebisha na makosa tuliyoyaona, tuna uhakika wa kushinda,"alisema Morocco.
Alisema pamoja kwamba anakwenda kushambulia zaidi kuliko kuzuia, lakini anaamini kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwani Guinea ni timu ngumu ambayo walikuwa nayo nchini Ivory Coast katika fainali za AFCON zilizopita
"Wachezaji wote wapo kwenye afya njema, hatutaki tena kufikiria mechi iliyopita, kule tumeshamaliza hakuna haja tena ya kuizungumzia, najua ni mechi ngumu tunakwenda kucheza dhidi ya Guinea, timu ambayo ilifanya vizuri AFCON iliyopita," alisema.
Naye kiungo wa timu hiyo, Novatus Dismas, alisema wamejifunza kutokana na mchezo uliopita kwani ulikuwa mgumu tofauti na walivyotegemea awali kama wachezaji, hivyo watakaza msuli ili kuhakikisha wanashinda mchezo ujao.
"Tumejifunza kutokana na mchezo uliopita, ulikuwa mgumu tofauti na tulivyotegemea, tumevifanyia kazi vitu ambavyo vilisababisha tukose ushindi mechi iliyopita, natumaini katika mechi inayokuja tutapata ushindi kwa sababu rekodi zinaonyesha tumekuwa tukipata matokeo mazuri tukicheza nje kuliko nyumbani,"alisema.
Mashabiki wengi wa soka walikosoa upangaji wa kikosi katika mchezo uliopita, wakidai kilikuwa na mabeki wengi zaidi kama vile timu ilikuwa inacheza ugenini na ilihitaji sare.
Kikosi cha Stars kiliondoka nchini usiku wa kuamkia jana kwenda Ivory Coast ambako mechi hiyo itachezwa, Uwanja wa Charles Konan Banny, Jumanne, saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED