BAO pekee la David Mwasa, juzi, liliiwezesha Mbeya City kuondoka na ushindi wa bao 1-0, katika mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Champioship dhidi ya Mbeya Kwanza, kwenye uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Ulikuwa mchezo mkali wa dabi ya Mbeya, kila timu ikitaka kudhihirisha kuwa ndiyo mbabe wa jijini hilo, lakini bao la nahodha huyo wa zamani wa Mbao FC, liliamua matokeo. Hii ni mechi ya kwanza kwa Mbeya City kupata ushindi kwenye ligi hiyo, baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 wiki iliyopita dhidi ya Bigman FC, ambayo zamani iliitwa Mwadui FC.
Kinakuwa kichapo cha pili kwa Mbeya Kwanza kwani mchezo wao wa raundi ya kwanza walipata kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Songea United, Uwanja wa Majimaji, Ruvuma. Kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, timu ya Mtibwa Sugar imeonekana haishikiki kwenye ligi hiyo, baada ya kupata ushindi wake wa pili mfululizo, ikiitwanga Cosmopolitan, mabao 2-0.
Mabao ya Mtibwa ambayo ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliopita, yaliwekwa wavuni na Omari Marungu, dakika ya tano ya mchezo, na Raizin Hafidh dakika ya 35.
Linakuwa ni bao la tatu kwa mchezaji huyo kwa michezo miwili tu ya Ligi ya Championship aliyocheza, kwani katika mechi ya ufunguzi wiki iliyopita, mabao mawili, Uwanja wa Manungu Complex, Turuani, Morogoro na kuipa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Green Warriors. Timu ya Stand United, ikiwa nyumbani, Uwanja wa Kambagare Shinyanga, imepata ushindi wa bao 1-0, likiwekwa wavuni na Andrew William.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED