KOCHA wa Timu ya KVZ FC, Ali Mohmed Ameir, amesema haridhishwi na matokeo anayoendelea kuyapata kwenye Ligi Kuu Zanzibar.
KVZ FC juzi ilipata sare nne mfululizo baada ya kufungana 1-1 katika mchezo wake wa tano dhidi ya Zimamoto SC, mchezo uliochezwa kwenye dimba la New Amaan Complex.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Ameir alisema kwamba, hakuna mwalimu anayeridhika na matokeo ya sare au kufungwa katika mchezo wanaohitaji alama tatu.
Alisema kikosi chake kimefanikiwa katika kukifanyia maboresho eneo la ulinzi na nafasi ya kati ambapo kumekuwa na muunganiko mzuri.
Alisema bado anakazi kubwa katika kufanyia maboresho eneo la ushambuliaji ili kuzitumia vizuri nafasi ambazo wanazipata.
“Tumefanikiwa kucheza vizuri katika nafasi ya ulinzi, lakini tunahitaji kufanya vizuri zaidi katika nafasi ya ushambuliaji bado hatupo vizuri, tunatengeneza njia na nafasi ya kushinda lakini washambuliaji wanashindwa kufunga,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED