Kanu aelezea machungu katika safari yake ya soka

By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Published at 10:36 AM Sep 15 2024
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitai ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko (kushoto), akizungumza na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kanu Heart Foundation, Nwanko Kanu (kulia) baada ya kutembelea hospitali hiyo kuwaona wagonjwa
PICHA: CHRISTINA MWAKANGALE
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitai ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko (kushoto), akizungumza na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kanu Heart Foundation, Nwanko Kanu (kulia) baada ya kutembelea hospitali hiyo kuwaona wagonjwa

NGULI wa soka Barani Afrika kutoka Nigeria aliyewahi kuzichezea klabu mbalimbali Ulaya, Nwankwo Kanu amesema akiwa mchezaji anakumbuka wakati mgumu aliopitia alipougua ugonjwa wa moyo na kulazimika kukaa nje kwa takribani mwaka mmoja.

Kanu, ambaye pia ni Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kanu Haert Foundation, amesema kutokana na kuwa miongoni mwa wenye tatizo hilo alianzisha taasisi hiyo nchini Nigeria ili kufanikisha huduma hasa upasuaji wa moyo.

Kanu, alisema hayo jana baada ya kutembelea wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dar es Salaam, wakiwamo watoto wenye maradhi ya moyo.

“Taasisi yangu nilianzisha mwaka 2000 na tayari watoto 690 wa Afrika wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua, ingawa upasuaji huu mara nyingi unafanyika nje ya nchi, hasa Israel, India na Uingereza,” alisema Kanu.

Alisema upasuaji huo kufanyika nje ya Nigeria ni ghali kutokana na watoto kuambatana na mzazi na huduma ya matibabu aina hiyo huwapasa kukaa nje kwa siku nyingi.

“Nimefika kwa sababu mimi ni kama nembo kwa wagonjwa hawa. Nakumbuka nikiwa mchezaji tatizo langu kubwa lilikuwa moyo, nilifanyiwa upasuaji Ohio huko Marekani. Nilikaa nje kwa mwaka mmoja,nilikuwa na hofu ya kutocheza tena soka, lakini nililirejea uwanjani nikiwa na nguvu na hata kushinda tuzo mbalimbali.

“Kuja hapa leo ni furaha kwangu. Ninawapongeza madaktari wote na kuwaombea wagonjwa, watambue kwamba wanaposikia Kanu, wajue kwamba nami nilipitia changamoto hiyo lakini nilisimamaimara,” alisema Kanu.