Fadlu aingia chimbo kuwasoma Walibya

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 11:15 AM Sep 08 2024
Kikosi cha Simba
Picha: Simba
Kikosi cha Simba

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameanza kazi ya kuifuatilia timu ya Al Ahly Tripoli ya Libya kujua habari zao na jinsi wanavyocheza ili kuwa na kazi rahisi ya kuidhibiti katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa Juni 11, jijini Tripoli, Jumapili ijayo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Fadlu, raia wa Afrika Kusini, alisema ameshaanza kuwasoma wapinzani wake ingawa bado anaendelea kuchimbua taarifa zao, uchezaji wao na mifumo wanayotumia ili iwe rahisi kukabiliana nao.

"Maandalizi hayajaisha, yanaendelea, tuna mambo mengi ya kufanya, kujiandaa sisi wenyewe mazoezini, lakini pia kuwasoma wapinzani wetu pia, ni siku chache tu tutaondoka kwenda kuwakabili.

Hatujapata kila kitu kutoka kwao, ila tuna taarifa chache ambazo zinaweza kutusaidia pa kuanzia,  lakini tunaendelea kuwasoma na kupata taarifa zao nyingi," alisema kocha hiyo.

Akiizungumzia mechi hiyo, Fadlu alisema itakuwa ngumu kutokana na Walibya hao wana timu nzuri, itakayocheza mbele ya mashabiki wao ambao kwa sasa wameruhusiwa kuingia viwanjani.

"Tuna mechi ngumu dhidi ya Al Ahly Tripoli nyumbani kwao, tunacheza mbele ya mashabiki wao ambao najua watawashangilia sana, lakini sisi hivi karibuni tulicheza mechi ya majaribio dhidi ya Al Hilal ya Sudan, imetusaidia sana, ulikuwa mchezo mzuri na kipimo tosha kwetu, imetuonyesha levo ya ushindani ambayo tunayo mpaka sasa," alisema.

Licha ya kwamba katika mchezo huo walitoka sare ya bao 1-1, lakini alifurahishwa na maendeleo ya wachezaji wake ambao wamesema kwa sasa wana utimamu wa mwili tofauti na mechi za mwanzo za Ngao ya Jamii

"Kwa sasa nafurahi kwa utimamu wa mwili ambao wachezaji wangu wanao, na hii ni tofauti na ilivyokuwa kwenye michezo wa Ngao ya Jamii, ambapo wengi wao hawakuwa nao, pia hawakuwa na pumzi za kucheza kwa dakika zote 90,"alisema Fadlu.

Kwa mara ya kwanza, kocha huyo amefunguka juu ya tuzo ya kocha bora ya mwezi Agosti aliyoipata, alisema anashukuru sana, lakini kwake haitakuwa bora kama asipolishukuru benchi lake la ufundi na wachezaji wake kwa ujumla

"Tuzo ya kocha bora siyo ya kwangu tu, bali ya benchi lote la ufundi ambao wananisaidia nyuma kuandaa yote haya pamoja na wafanyakazi wengine, na wachezaji wangu ambao wamefanya kazi kubwa, fikiria tumefunga mabao saba, lakini hatukuwaacha wapinzani wetu wapige shuti hata moja lililolenga lango, hii inaonesha kuwa upande wa beki pamoja na kipa umefanyiwa kazi vizuri, lakini kule mbele tunatakiwa kuongeza juhudi, tumefunga mabao yetu matano baada ya mapumziko, lakini inatubidi tupambane zaidi," alisema kocha huyo.