Che Malone: Tutawashangaza Al Ahly

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 10:31 AM Sep 15 2024
Che Malone: Tutawashangaza Al Ahly
Picha: Simba
Che Malone: Tutawashangaza Al Ahly

BEKI kisiki wa Simba, Che Fondoh Malone, amesema yeye na wachezaji wenzake wapo tayari kwa mchezo wa leo wa raundi ya kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya na watawashangaza wapinzani wao hao.

Akizungumza kutoka nchini humo ambako mchezo wa mkondo wa kwanza utachezwa kwenye uwanja wa Juni 11, jijini Tripoli, Che Malone amesema wanataka kushinda si mchezo wa kesho tu, bali yote ambayo timu yao itakabiliana nayo katika mechi za Kombe la Shirikisho.

"Mimi niko tayari na hata wenzangu wapo tayari, kwa mechi ya ya kesho (leo), najua haitokuwa rahisi, ni kweli hii si Ligi ya Mabingwa, ni Kombe la Shirikisho, lakini huwezi kudharau kwa sababu mara nyingi ni timu zile zile za kiwango kile kile zinazocheza michuano yote miwili kila msimu, tutawashangaza wapinzani wetu, tumekuja kupambana kupata ushindi," alisema Che Malone.

Alisema maandalizi ya mchezo huo hayakuanza hivi karibuni, au kwenye mapumziko ya kalenda za FIFA, bali mwanzoni mwa msimu.

"Maandalizi yamekamilika kwa sababu yalianza zamani, hayajaanza sasa, siwezi kusema eti yamefanyika kipindi cha mapumziko ya FIFA hapana, yalianza kabla ya msimu.

Malengo ya klabu yameshawekwa wazi, hivyo sisi wachezaji tunachofanya ni kuyafanyia kazi, tulicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan timu ambayo mara nyingi inafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na wakati mwingine inacheza nusu fainali, kilikua kipimo tosha kwa sababu wachezaji wengine ambao hawakuwahi kucheza michuano ya CAF, ilikuwa ni nafasi nzuri ya kujionea mambo yanavyokuwa," alisema.

Alisema pamoja na kwamba Simba ina rekodi nzuri ya michezo ya kimataifa, lakini wao hawaangalii hilo, badala yake watalazimika kupambana ili kutimiza malengo.

"Tunahitajika kupambana na kushinda kila mechi inayokuja kwa sababu kufuzu michuano ya CAF siyo jambo rahisi, tunakwenda kucheza mechi na kushinda kwa ajili ya kupambania kombe, tunajiamini na nadhani kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa," alisema.

Mchezo huo unatarajiwa kuanza majira ya saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na timu hizo zitarudiana wiki ijayo jijini Dar es salaam. 

Huu utakuwa mchezo wa kwanza wa kimataifa msimu huu kwa Simba, kwani haikucheza mechi yoyote hatua ya awali kutokana kuwa kwenye kiwango cha juu ndani ya 10 bora Afrika, ambapo imekuwa na faida ya kutocheza michezo ya awali, badala yake kwenda moja kwa moja raundi ya kwanza.