BAO alilofunga Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya dhidi ya KenGold, limempa kiburi beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Hamad 'Bacca', akisema ndoto yake sasa ni kuwa na mwendelezo wa kufunga mabao kwa ajili ya kusaka ufungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Bacca, alisema bao alilofunga dhidi ya KenGold limempa chachu ya kuendela kupachika mabao, hivyo kuwataka mastraika wa Ligi Kuu kuwa makini, kwani ameingia rasmi kwenye mapambano ya kuwania kiatu.
"Lile bao limeniamsha, tayari nimeshaanza kuona inawezekana kabisa kupambania ufungaji bora, na ni malengo yangu siku moja kuwa beki ninayefukuzana na mastraika kuwania kiatu, ikiwezekana nikipate kabisa ingawa najua si rahisi.
Kwa ligi yetu hii ukifikisha mabao 15 tu tayari mfungaji bora, nawaambia kina Prince Dube na wenzake, safari hii na mimi nipo, wacha tuone," alisema beki huyo.
Lilikuwa ni bao pekee kwenye mchezo huo, Yanga ikishinda bao 1-0, lakini pia ni la kwanza kwa beki huyo tangu alipojiunga na Yanga 2022, akitokea KMKM ya Zanzibar, na kuongezewa mkataba mpya mwaka jana unaomuweka Jangwani hadi mwaka 2027.
"Najisikia furaha sana kufunga bao langu la kwanza nikiwa Yanga, nataka kuwa na mwendelezo sasa wa kufunga, nimeona raha ya kupachika mabao nitakuwa najituma zaidi ili niendelee kufunga.
Nadhani mpaka sasa kwenye orodha ya wafungaji hakuna aliyefikisha mabao matano na kama ndiyo hivyo ngoja niongeze nguvu ya kupambania kiatu mwisho wa msimu," alisema.
Aidha, alisema kinachompa nguvu hiyo ni jinsi walivyojifunza mazoezini kumalizia mipira ya adhabu kwa wapinzani, hivyo anaona atafunga sana.
"Nilivyofunga mimi lile bao siyo kama ilikuwa bahati, tulifanya mazoezi jinsi ya kupiga mipira ya faulo na kufunga na hasa sisi mabeki unajua tumezoea sana mara kwa mara kuruka, hivyo inakuwa rahisi kwenda juu kuuwania mpira,kwa maana hiyo wala sikushangaa nilipofunga kwa sababu tulijua itatokea tu kama siyo kwenye mchezo ule, basi mwingine, na utakuwa ni mwendelezo wetu," alisema beki huyo
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED