Umakini unahitajika katika utekelezaji bajeti 2024/25

Nipashe Jumapili
Published at 12:21 PM Jun 30 2024
Bunge la Tanzania.
Picha: Maktaba
Bunge la Tanzania.

BAJETI ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 itafikia ukomo wake kesho, hivyo kuanza mwaka mpya wa fedha 2024/25 ambao serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh. Sh. trilioni 49.35

Katika bajeti hiyo ambayo ni ya nne kwa serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kunatarajiwa ongezeko la makusanyo na matumizi kwa asilimia 11.2 kulinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha, ongezeko la bajeti kwa kiasi kikubwa limetokana na kugharamia: Deni la Serikali ambalo limeongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi, kuongezeka kwa viwango vya riba na kuiva kwa mikopo ya zamani.

Vilevile, ajira mpya; ulipaji wa hati za madai; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025; na maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ikiwamo ujenzi na ukarabati wa viwanja vinatajwa kuchangia ongezeko hilo.

Sura ya bajeti hiyo inaonesha kuwa mapato ya ndani - Serikali Kuu yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 33.254, misaada na mikopo nafuu kutoka washirika wa maendeleo Sh. trilioni 5.131 na mikopo ya kibiashara ndani na nje Sh. trilioni 9.604. 

Kati ya Sh. trilioni 49.35 zinazotarajiwa kukusanywa na kutumika, matumizi ya kawaida yanatarajiwa kuwa trilioni 34.590 na matumizi ya maendeleo Sh. trilioni 14.755.

Ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza utekelezaji bajeti hiyo, Nipashe Jumapili tunakumbusha serikali umuhimu wa kuzingatia vipaumbele vilivyoanishwa katika bajeti hiyo.

Hivyo ni pamoja na kukamilisha miradi ya kielelezo na ya kimkakati, kuimarisha rasilimali watu hasa katika sekta za huduma za jamii, kuongeza matumizi ya TEHAMA na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji katika sekta binafsi.

Tunakumbusha pia serikali kuimarisha upatikanaji mbegu bora, pembejeo na zana za kilimo na uvuvi, huduma za ugani na utafiti, uimarishaji malambo na majosho, ujenzi wa maghala na upatikanaji masoko ya mazao na mifugo ndani na nje ya nchi.

Serikali pia imepanga kufungamanisha ukuaji uchumi na maendeleo ya watu kwa kuboresha upatikanaji huduma za afya, elimu na ujuzi na huduma za maji safi na salama kupitia utoaji elimumsingi bila ada, utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati, kuboresha huduma ya maji, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ununuzi na usambazaji dawa pamoja na ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya.

Nipashe Jumapili tunakumbusha pia uboreshaji mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu nishati, usafirishaji pamoja na ununuzi na ukarabati wa ndege, meli na vivuko.

Mbali na vipaumbele hivyo, serikali pia inatarajiwa kupunguza tatizo la ajira nchini kwa kutoa ajira mpya kwa wananchi, hususan vijana waliohitimu vyuo vikuu na maeneo mengine ya kitaaluma.

Vilevile, tunakumbusha ahadi iliyotolewa ya kulipa madeni ya wazabuni, watumishi na mifuko ya hifadhi ya jamii ambako Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebainisha kuwapo kwa deni kubwa na la muda mrefu.

Nipashe Jumapili tunaamini kuwa, bila kuwapo nidhamu katika matumizi, utekelezaji bajeti hiyo ya serikali hautafanikiwa, hivyo kuna haja serikali kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha utawala bora katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.  

Ndiyo maana tunasisitiza mamlaka husika za serikali kuongeza umakini katika kuyatekeleza mambo haya muhimu yaliyopangwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2024/25.