Elimu ya malipo mtandao ihusishe wananchi wote

Nipashe Jumapili
Published at 09:16 AM Jun 16 2024
Waziri wa Fedha, Dk,. Mwigulu nchemba.
Picha: Mtandao
Waziri wa Fedha, Dk,. Mwigulu nchemba.

WAZIRI wa Fedha, Dk,. Mwigulu nchemba, Alhamisi wiki hii, aliwasilisha mapendekezo ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2024/25 jijini Dodoma. Katika mapendekezo hayo, serikali imepanga kutumia Sh. trilioni 49.35 kwa ajili ya matumizi ya kawaida kwa shughuli za serikali na miradi ya maendeleo.

Baada ya kuwasilishwa kwa mapendekezo hayo, wabunge kuanzia Jumanne wanatarajia kujadili na hatimaye kupitishwa na kwa mujibu wa kanuni za bunge, ili bajeti ipite, inatakiwa  mbunge kupiga kura kwa kusema NDIYO au HAPANA. 

Kwa kawaida, hakuna bajeti ya serikali iliyowahi kukwama kwa wabunge kuikataa isipokuwa makadirio ya mapato na matumizi ya zilizokuwa wizara za miundombinu, na nishati na madini wakati wa serikali ya awamu ya nne, kwa mawaziri husika kutakiwa wakajipange upya kutokana na kukosa uhalisia. 

Wakati wa kuwasilisha mapendekezo hayo ambayo bajeti ya mwaka ujao wa fedha imepokewa kwa hisia chanya na Watanzania wengi, mkazo mkubwa alioutoa Waziri Nchemba ni kuongeza ukusanyaji mapato kwa ajili ya kupata fedha zitakazowezesha serikali kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ya shughuli za kila siku ikiwamo ulipaji wa mishahara na stahiki kwa watumishi wa umma. 

Katika kusisitiza hilo, Dk. Nchemba alisema nguvu kubwa itaelekezwa katika matumizi ya risiti na malipo ya kidijitali kwenye miamala mbalimbali. Hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti kuvuja kwa mapato ya serikali, hivyo kuwezesha kuongezeka kwa fedha katika mfuko wa serikali. 

Licha ya kusisitiza mfumo huo, Waziri Nchemba pia alisema watahimiza malipo mengi ya serikali kufanyika kwa njia ya mtandao tofauti na sasa ambapo mfumo wa malipo ni kwa fedha taslimu.

Mkazo mkubwa katika hilo ni kuwezesha kuwapo kwa usalama wa fedha za wananchi na serikali kwa ujumla pamoja na kuendana na mabadiliko ya sasa ya sayansi na teknolojia ambayo yanahusisha pia miamala mbalimbali. 

Lengo la kufanya hivyo, alisema ni kuwa na mfumo wa uchumi usiotumia fedha taslimu (cash less economy) ambao pia unaokoa muda wa mtu kufanya miamala popote alipo bila kwenda benki au kununua bidhaa sehemu fulani.  Kwa kutumia mfumo huo, mtu anaweza kulipia bidhaa au huduma kama vile kukata tiketi ya ndege, meli au gari bila Kwenda kwenye ofisi husika. 

Wazo la kufanya malipo kwa njia  ya mtandao ni jema kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo ni mfumo wa kidunia na Tanzania haiwezi kujitenga. Wahenga wanasema maendeleo hayo yaliyochagizwa na utandawazi ni sawa na mafuriko ambayo mtu hawezi kuyazua kwa kutumia viganja vya mikono yake. Kwa mantiki hiyo, Watanzania watake wasitake ni lazima wakubali na kuwa katika mfumo rasmi.

Pamoja na ukweli huo, kwa sasa ni Watanzania wachache wanaotumia mifumo rasmi ya huduma za kifedha kama vile benki na malipo kwa njia ya mitandao ya simu. Kutokana na hali hiyo,  elimu kuhusu matumizi ya kifedha kwa njia jumuishi inapaswa kutolewa kwa wananchi wote ili kushiriki kikamilifu katika hilo. 

Kama ambavyo hivi karibuni timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha wakishirikina na maofisa wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wamekuwa wakipita mikoani kutoa elimu kuhusu mikopo maarufu kama kausha damu au mikopo umiza, suala la malipo mtandao halina budi kupewa kipaumbele.