Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu ) Jenista Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho amesema serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imetenga kiasi cha milioni 500 kwa mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya Ujenzi wa kituko cha afya katika Kijiji cha Nguvu moja.
Amesema hayo jana wakati alipopita kuwasalimia wananchi katika Kijiji cha Peramiho A kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Aliongeza kusema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama kinachohangaika na matatizo ya wananchi."Nimekuja na bati mia mbili (200) kwa ajili ya ujenzi wa soko, tunataka kuona kila mtu anajishughulisha katika shughuli za uchumi," alisema na kuongea kuwa;
"Naomba viongozi wa soko, bati hizi zisitumike vibaya na natoa fedha kiasi cha shilingi milioni moja ili muanze kupiga ripu soko letu.Natoa shilingi milioni moja nyingine kuwapa kikundi cha hamasa, na fedha nyingine ni kwa ajili ya timu za mpira kama ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyoeleza katika kukuza vipaji vya vijana wetu na kuwapa shilingi milioni moja nyingine vijana wa boda boda, fedha zote zitawekwa katika akaunti maalumu ya vikundi hivyo," alisema
Waziri Mhagama alihimiza wananchi kuendelea kuchangamkia fursa za uchumi zinazojitokeza katika halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine Godfrey Mukanula, aliyekuwa mmoja wa makamanda wa upinzani kutoka CHADEMA,katika Jimbo la Peramiho alijiunga na CCM.
Akizungumzia kuhusu uwaumuzi wake wa kuhama chama, Mukanula alisema mambo ya maendeleo yanayofanywa na Mbunge wa Peramiho yamemhamasisha kuzaliwa upya katika Chama Cha Mapinduzi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED