Magu washiriki apokezi ya Mwenge a Uhuru Mwanza

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:51 PM Oct 06 2024
Magu washiriki apokezi ya Mwenge a Uhuru Mwanza
Picha:Mpigapicha Wetu
Magu washiriki apokezi ya Mwenge a Uhuru Mwanza

MKUU wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari leo Oktoba,06, 2024 amewaongoza viongozi na watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo kuupokea Mwenge wa Uhuru ambao umetokea mkoani Geita na kupokewa katika Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza.

Mbali na shamrashamra za kuupokea Mwenge huo zilizoanza mapema saa 11: 00 asubuhi, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ndiye aliyekabidhiwa Mwenge huo na Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela.

Akizungumza kwenye mapokezi hayo yaliyofanyika kwenye kijiji cha Nyamadoke Halmashauri ya Buchosa wilayani, Sengerema, Mtanda amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya 7 na Halmashauri 8 katika umbali wa zaidi ya kilometa 649.

Amesema Mwenge huo utatembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 58 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya bilioni 98.

Ametaja miradi hiyo kuwa inahusu sekta za maji, elimu, afya, kilimo na miundombinu hasa ikizingatiwa mkoa huo wa Mwanza unachangia pato la Taifa kwa asilimia 7.2.

1

Naye Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava amesema anatarajia kuona miradi hiyo katika mkoa wa Mwanza ikiwa kwenye ubora wa kuridhisha huku ile ambayo itawekwa mawe ya uzinduzi akitarajia kuwa itakamilika kwa wakati.

Tayari mkuu wa mkoa wa Mwanza amemkabidhi Mwenge huo wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Seni Ngaga kwa ajili ya kukimbiza kwenye halmashauri ya Buchosa leo tarehe 6 Oktoba 2024.
Mbio za Mwenge mwaka huu zinaongozwa na kauli mbiu isemayo; "Tunza mazingira, "Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu".