NI takribani wiki tatu sasa wananchi wa Mji wa Lindi wanahaha kutafuta maji safi na salama, kutokana na huduma hiyo kutopatikana .
Mji huo unategemea maji kutoka vyanzo vya Kitunda, Mmongo na Liwayawaya na bado kiasi kinachopatikana kimeshindwa kukidhi mahitaji.
Nipashe Digital alitembelea baadhi ya maeneo na kubaini kukumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Mitema, Banduka Kata ya Rasbura, Mlandege, Sabasaba Kata ya Jamhuri.
Wakizungumzia kadhia hiyo Salima Yusufu,Juma Daudi, Hemedi Saidi na Ezekiel Mathias wamedai zaidi ya wiki tatu sasa hawajapata huduma hiyo kutoka Mamlaka ya Maji Safi, Salama na Mazingira mji Lindi (LUWASA).
‘’Tangu Septemba mosi hadi leo Oktoba 5,2024 hatujapata maji katika maeneo yetu,”walisema.
Aidha,wamedai licha ya Serikali kujenga mradi mkubwa wa maji kutoka chanzo kilichopo Kata ya Ng’apa na viongozi kuahidi kukamilika kwake ni mwarobaini wa tatizo hilo kwa Mji wa Lindi, bado hali inaonekana kutokuwa mkombozi kwa wananchi.
Wananchi hao wamesema licha ya viongozi wao wenyeviti wa mitaa kufuatilia mamlaka husika kufahamu tatizo linalochangia kutopata huduma hiyo katika maeneo yao, wamedai kupewa maelezo yakiwemo tatizo la umeme, ubovu wa miundombinu na kupungua kwa maji chanzo cha Ng’apa.
Pia wamedai kutokana na tatizo hilo, wanalazimika kutumia maji kutoka kwenye mifereji, ambayo siyo salama kwa matumizi ya binadamu kutokana na kuchanganyika na wadudu wakali wakiwemo nyoka wakijivinjali ndani ya mifereji hiyo.
Baadhi ya viongozi wa Mitaa hiyo,Justin Mrope (Mitema), Ally Yusufu (Sabasaba) na Daud Juma (Banduka) wakizungumza kwa niaba ya wenzao wamekiri kwenda mamlaka husika kutaka kufahamu tatizo linalochangia kukosa maji kwenye mitaa yao kwa muda mrefu.
“Ni kweli tulifika LUWASA kufahamu tatizo, lakini tumeelezwa sababu za umeme,kuharibika Bomba linalopeleka maji kwetu na kupungua Maji chanzo cha Ng’apa,”wamesema.
Mwandishi alipowasiliana na Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Maji Mji wa Lindi (LUWASA), Juma Soud alithibitisha kuwepo kwa tatizo hilo na kueleza linatarajia kuondoka muda mfupi ujao,baada ya mkandarasi kupata vifaa.
“Ni kweli tatizo hilo limechukuwea muda mrefu kutokana na mkandarasi kuchelewa kupata vifaa,lakini sasa tayari kati ya kesho au keshokutwa vitakuwa vimewasili,”amesema Soud.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED