SERIKALI imesema kitendo chake cha kumfukuza Kiongozi na Mchungaji wa Kanisa la Christian Life maarufu kama Kiboko ya Wachawi, Dominique Dibwe, kilikuwa sahihi kwa sababu mhusika amedhihirisha utapeli kupitia video mbalimbali zilizoko mtandaoni.
Katika mitandao ya kijamii kumesambaa video fupi za mchungaji huyo ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zenye maudhui ya kejeli akionekana akihesabu fedha, huku akisema bado anakumbuka Sh. 500,000 alizokuwa akiwatoza waumini wake ili kuwaombea.
Julai 25, mwaka huu, serikali kupitia Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa, ilimwandikia barua mchungaji huyo kumtaka kufunga shughuli na huduma alizokuwa akiziendesha huko Buza, Temeke mkoani Dar es Salaam, agizo ambalo lilitekelezwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, aliyasema hayo jana wakati akifunga makambi yaliyoandaliwa na Kanisa la Waadventista Wasabato Maranatha katika Mtaa wa Majani ya Chai, Arumeru, mkoani Arusha kwamba walimwondoa mchungaji huyo kutokana na kukiuka sheria ya usajili.
“Nimeshuhudia huko alikokwenda amekuwa akisambaza klipu za video kuthibitisha kwamba aliyokuwa akifanya ni kinyume kabisa na mafundisho ya kitabu cha dini.
“Ikiwamo suala la kutapeli watu, kuwatoza fedha nje ya utaratibu, kuwaaminisha watu kwamba miujiza inaweza kuwafanya wawe matajiri au wapate ufumbuzi wa matatizo yao, mambo ambayo ni kinyume na mafundisho ya dini zetu” alisema.
Masauni alipongeza Kanisa la Waadventista Wasabato kwamba wao si sehemu ya wanaohubiri mambo kama hayo.
Aliwapongeza kwa kusimamia misingi sahihi ya vitabu vya dini na kutoa wito kwa watu walioingia katika shughuli za kidini, kufuata misingi ya kisheria inayolenga kuhakikisha inafuata mafundisho sahihi ya vitabu vya dini.
“Uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa katiba upo, lakini hautakiwi kuvuka mipaka na kuvunja sheria za nchi si kwa wageni hata wenyeji. “Ziko sheria lazima zifuatwe zimetungwa kwa ajili ya maslahi ya wananchi wa taifa hili,” alisema.
MAUAJI NA UTEKAJI
Pia alisema suala la maadili kwa vijana ni muhimu, akibainisha katika kipindi cha mwezi Agosti hadi sasa, wameshuhudia ongezeko la matukio mabaya yanayohusu mauaji ya kikatili yanayohusishwa na masuala mbalimbali, ikiwamo imani za kishirikina.
“Tumesikia mauaji yaliyochanganyika na uhalifu mwingine ukiwamo ubakaji, uuaji wa kutumia silaha za jadi na upoteaji. Imechukua kazi kubwa sana vyombo vyetu vya usalama kufanya udhibiti wa jambo hilo, yote yanachangiwa na mmomonyoko wa maadili.
“Hakuna hata mtu mmoja ambaye ana hofu ya Mungu ambaye atafanya kitendo chochote kiovu kinacholenga kuleta athari au madhara kwa watu wengine. Dini zote zinakataza,” alisema.
Hivi karibuni, Jeshi la Polisi lilitangaza kuwashikilia watu kadhaa akiwamo mganga wa kienyeji huku miili 10 ikibainika baadhi kuzikwa kwa mfumo wa kukaa wakiwamo watoto wa watuhumiwa, baada ya watu hao kuripotiwa kupotea na wengine kutekwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED