Wafugaji chanzo migongano binadamu, wanyamapori

By Jenifer Gilla , Nipashe Jumapili
Published at 12:47 PM Sep 29 2024
Wafugaji chanzo migongano binadamu, wanyamapori
Picha:Mtandao
Wafugaji chanzo migongano binadamu, wanyamapori

WAKAZI wa Kijiji cha Mtelawamwahi, Kata ya Ligera, Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, wameiomba serikali kudhibiti wafugaji wanaolisha mifugo ndani ya hifadhi kutokana na kusaba bisha ongezeko la migongano kati ya binadamu na wanyamapori.

Walisema tangu wafugaji hao walipoingia katika kijiji hicho na kulisha mifugo yao katika hifadhi migongano baina yao na wanyamapori imeongezeka kwa sababu idadi kubwa ya tembo wame ondoka kwenye makazi yao na kuhamia kijijini hapo wakiikimbia mifugo hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania ( JET) wakazi hao walisema hali hiyo inasababisha uharibifu mkubwa wa mazao yao kwa kuwa idadi kubwa ya tembo wanavamia mashamba tofauti na awali.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Rajabu Athumani, alisema wafugaji wanavyoongezeka ndivyo uharibifu wa mashamba unavyoongezeka na kutoa mfano mwaka jana walipokea kesi za malalamiko ya kuvamiwa masham ba kutoka kwa wakulima wanane, lakini mwaka huu zimefikia 14.

Alisema serikali ya kijiji kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi likiwamo Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), wanatoa elimu kwa wanakijiji namna ya kupunguza migongano hiyo kama vile kutofanya shughuli za kibinadamu karibu na hifadhi.

Alisema shirika la GIZ pia linawasaidia kuwapa elimu ya kutengeneza dawa zenye harufu kali kwa ajili ya kuzuia tembo kuingia kwenye mashamba yao hali iliyopunguza uharibifu kwa kiasi kikubwa. Alisema kama wafugaji wataendelea kulisha mifugo katika hifadhi, tembo wataendelea kuvamia mashamba na kwamba kunahitajika hatua za haraka za kuwaondoa watu hao.

“Kama unavyojua tembo ni mnyama mwenye akili sana, ukimwekea dawa katika shamba hili, kesho anahamia shamba la upande mwingine, pia ana uwezo wa kubuni njia mpya za uharibifu kila siku, kwa hiyo tunaomba serikali itusaidie kuwaondoa hawa wafugaji,” alisema.

Mtendaji wa kijiji hicho, Joseph Haule alisema kabla ya wafugaji hao, uharibifu wa mashamba haukuwa mkubwa, tembo wakiharibu robo heka ya shamba, lakini sasa wamekuwa wengi na kuharibu heka tatu za mkulima mmoja.

Askari wa wanyamapori wa kijiji hicho (VGS), Musa Nchimbi, aliiomba serikali na GIZ kuwaongezea idadi ya askari kwa kuwa wapo wa chache na tembo wanazidi kuongezeka.

Aliomba pia kuwasaidia vitendea kazi zikiwamo pikipiki, viatu, mabomu ya kisasa ya kufukuzia wanyama ili kuwarahishia kazi pamoja na kuwalipa posho ili kuwapa nguvu ya kutekeleza majukumu yao kwa kuwa kazi hiyo wanaifanya kwa kujitolea.

Mkulima wa mahindi, John Mhagama, alisema elimu zaidi inahitajika ili kuwahamisha wafugaji na wakulima wanofanya shughuli zao karibu na hifadhi na hawana sababu yoyote ya msingi inayowapeleka katika maeneo hayo.

Alisema kuwapo kwa watu hao katika hifadhi pia Kunachochea shughuli za ujangiri wa wanyama pori ambao wanatumia mwanya huo kutekeleza shughuli zao.

Alisema mwaka jana tembo walivamia shamba lake la mahindi na kuharibu heka mbili ikimwacha na umasikini mkubwa na kulazimika kutafuta pesa za kumwezesha kulima mwaka huu.

Mhifadhi wa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Issa Hassan Ndomondo, alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi wanafanya juhudi kubwa kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori katika vijiji vilivyopakana na hifadhi katika wilaya hiyo. Alisema wanatoa elimu kwa wafugaji ya namna ya kujikinga na wanyama waharibifu, kuwapa dawa za kufukuza wanyama wao pamoja na kuongeza nguvu kazi ya VGS kwa kuwapa mafunzo na mbinu mpya za kukabiliana na wanyamapori waharibifu katika maeneo yao.

Migongano hiyo inachochewa na wananchi kutokuwa na uelewa wa namna ya kujikinga na wanyamapori waharibifu na utayari wa kuwakubali wanyama hao na kuishi nao kwa tahadhari.

Mtelawamwahi ni moja ya vijiji vilivyo karibu na mapitio ya wanyamapori ya Selous-Niassa yanayounganisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Hifadhi ya Niassa ya nchini Msumbiji.