MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, (IGP) Camillus Wambura, amepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. Milioni 235.5 kutoka Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS Ltd) vitakavyoisaidia Hospitali ya Rufaa ya Polisi Kilwa Road.
Msaada huo umejumuisha mashine ya x-ray ya kisasa, vifaa vya maabara, vya mazoezi tiba na vya wodini vitakavyotumika kulazia wagonjwa vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 235,5.
Akizungumza leo katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, IGP Wambura amesema msaada huo umefika wakati muafaka ambao Jeshi la Polisi lipo katika hatua mbalimbali za maboresho ikiwemo kuhakikisha askari wake wanapata huduma bora za afya.
"Vifaa tiba hivi vitaendelea kusaidia kupanua wigo wa utoaji huduma katika vituo tiba vyetu kwa watumishi wa Jeshi la Polisi, familia zao na wananchi kwa ujumla," amesema IGP Wambura.
Mwenyekiti wa Bodi ya URA SACCOS ambaye pia ni Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu (CP) Suzan Kaganda, amesema URA SACCOS imekuwa na utaratibu wa kutenga fedha kutokana na ziada inayopatikana na kuirudisha kwa jamii kwa mujibu wa sheria na kanuni za kiushirika.
CP Kaganda amesema kuanzia mwaka 2017 ulipoanza utaratibu huo chama hicho cha ushirika kimeshatoa kwa jamii vifaa tiba vyenye thamani zaidi ya Sh. Milioni 581 kwa lengo la kupunguza changamoto za kitabibu.
"Ushirika unaamini huduma ya Hospitali sio tuu inawanufaisha askari lakini pia jamii ya watanzania wanaohudumiwa kwenye hospitali zetu. Hivyo kuleta maana halisi ya kurudisha kwa jamii na kuihudumia kupitia vifaa tiba hivyo," amesema CP Kaganda.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dar es Salaam Anjela Nalimi ameipongeza URA SACCOS akieleza kuwa hiyo iwe ni chachu kwa vyama vingine vya ushirika kuiga mfano huo kwa kutumia sehemu za fedha za ziada kuijali jamii.
Msaada huo wa vifaa tiba unakwenda kutumika katika hospitali ya Kilwa road na zahanati sita za Polisi ambazo ni Zahanati ya Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Zahanati ya shule ya Polisi Moshi, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Mtwara, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Tanga, Zahanati ya Polisi Mkoa wa Dodoma na Zahanati ya Polisi Mkoa Kaskazini Pemba.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED