Sindano, pedi zaokotwa ufukweni mwa bahari

By Enock Charles , Nipashe Jumapili
Published at 08:48 AM Sep 29 2024
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisutu, wakifanya usafi katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, eneo la daraja la Selander kwa kushirikiana na taasisi ya Sanamare, jijini Dar es Salaam jana.
PICHA:ENOCK CHARLES
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisutu, wakifanya usafi katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, eneo la daraja la Selander kwa kushirikiana na taasisi ya Sanamare, jijini Dar es Salaam jana.

WADAU wa mazingira nchini waliojitokeza kusafisha ufukwe wa Bahari ya Hindi, wamekutana na sindano za hospitalini, pedi, plastiki za aina mbalimbali na nguo.

Kutokana na hali hiyo, wameitaka jamii kujenga utamaduni wa kulinda fukwe hizo na viumbe hai vilivyoko baharini na kuepuka mlipuko wa magonjwa unaoweza kutokea kutokana na uchafu.

Katibu wa Mipango wa Taasisi ya Sanamare, Pius Mollel, aliyasema hayo jana wakati wa zoezi la usafi katika fukwe hizo lililoshirikisha taasisi mbalimbali za mazingira na Shule ya Sekondari Kisutu waliosafisha  ufukwe wa Selander Bridge, jijini Dar es Salaam.

Mollel alisema hali ya usafi katika fukwe walizotembelea jijini humo sio nzuri na kuomba wadau kuungana kuzisafisha mara kwa mara na kuzitunza.

“Leo tumekusanya taka mifuko zaidi ya 150 ambazo ni mchanganyiko wa vitu mbalimbali kama vile za hospitalini ikiwamo sindano, pedi za watoto, plastiki za aina mbalimbali na nguo za aina mbalimbali, vitu ambavyo havitakiwi katika fukwe zetu.

“Lakini hatujaishia hapo pia, tunachukua taarifa ya aina ya taka zinazopatikana hapa kwa wingi na chapa zilizoongoza kwa uchafuzi wa taka. Hii inasaidia kujua chanzo cha taka zinazopatikana ambazo tutazipeleka kwa mamlaka husika ili hatua mbalimbali zichukuliwe, “ alisema.

Alipendekeza wahusika watakaopatikana kuwa bidhaa zao zinaongoza kwa kuzalisha taka hizo, wawajibike ili kupunguza athari katika fukwe nchini.

Pia alipendekeza kuanzisha mipango ya kurejeleza taka hizo (recycling) au kutoa fedha kwa mashirika ya kufanya usafi wa mazingira ili kuzipunguza.

Mwalimu wa Mazingira wa Shule ya Sekondari Kisutu, Anaely Mwakyeja, alisema kuna umuhimu wa elimu ya mazingira kutolewa kwa vijana katika shule za msingi na sekondari ili kujenga kizazi kinachojali mazingira kwa miaka ijayo.

“Tatizo hili la uchafu katika fukwe zetu pamoja na mambo mengine, linatokana na tabia binafsi za watu na kukosa uelewa wa elimu ya mazingira sasa tukiwafundisha wanafunzi kama hivi, tutajenga kizazi kilichostaarabika na kuheshimu mazingira.

“Kwa taka hizi kuna uwezekano wa kudhuru binadamu na wanyama hasa viumbehai wanaoishi ndani ya bahari mfano, humu tumekuta sindano, pengine ni za vijana wanaotumia madawa ya kulevya na wanazitupa tu kwa sababu hawajui umuhimu wa Bahari,” alisema.

Mwalimu huyo pia, aliziomba mamlaka za serikali za mitaa kuzisimamia fukwe zilizoko katika maeneo yao kwa kuandaa siku maalum za usafi na kuhamasisha wananchi kuzipenda fukwe hizo kwa kuzifanyia usafi kila wakati.

“Fukwe nyingi zina serikali yake ya mtaa ninatamani sana zihamasishe jamii kuungana pamoja na hizi taasisi tofauti kuratibu kila mwezi kuwa na usafi kama huu wa leo,” alisema.

Alisema kwa kufanya hivyo itakuwa ni njia rahisi kufanya bahari kuwa safi kwa sababu taka walizokusanya zinaonesha ni za muda mrefu.