Samia asema hajawahi kuua mtu

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 07:57 AM Sep 29 2024

Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha:Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema katika maisha yake hajawahi kuua mtu labda sisimizi, huku akiwataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwajibu wale wote ambao wamekuwa wakimshambulia kwa maneno, ikiwamo kumwita muuaji.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akihutubia wanachama wa chama hicho pamoja na viongozi wa serikali katika sherehe za kilele cha Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Rais Samia alisema amesikia maneno hayo na kwa masikitiko makubwa kwa namna anavyoshambuliwa kuwa yeye ni muuaji ilhali hajawahi kuua mtu.

“Sisimizi nimeua lakini mtu sijawahi, sijawahi kuua. Sasa ombi langu kwenu ni kusimama imara. Ukweli  mnaujua mdomo wa Mwenyekiti mmoja kujibu hoja zile hauwezi, pengine mwenyekiti wakati mambo haya yanatokea ninakuwa katika majukumu mengine.

“Kwa hiyo msimame muwajibu. Ndugu  zangu, mnahofia nini? Hakuna cha kuhofia hapa. Mkiambiwa  Mwenyekiti na Rais wenu muuaji, waambieni kweli ameua nguvu za upinzani. Ameua  njia zote za kuzidisha umaskini ndani ya nchi yetu, amekuza uchumi wa nchi hii na ameua mambo hasi ya kuturudisha nyuma,”alisema.

Rais Samia alisema kweli ameua giza lililokuwa limeigubika nchi na kwamba, sasa nchi inang’ara kimataifa na hayo ndiyo mambo ambayo ameua na si mtu.

Alisema wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani, wanachama wa CCM wanapaswa kushikamana kuwa kitu kimoja ili kushinda kwa kishindo.

“Kamati za ushindi mnazoziweka hivi sasa lazima ziwe kwa ajili ya kukivusha chama na siyo watu, kwani haya mambo ndiyo yameturudisha nyuma kutokana na kuunda kamati za kuvusha watu, badala ya kuvusha chama,” alisema Rais Samia.

Vilevile, alisema anafahamu hivi sasa watu tayari wameanza kujipanga kwa vitenge na fedha kwa ajili ya kutoa kwa wapigakura, lakini kinachopaswa kuzingatiwa ni kuwaunga mkono watu wenye sifa na siyo vinginevyo.

CCM HAINA MBADALA

Rais Samia alisema: “Tunapaswa kuunga mkono watu wenye sifa siyo kwa ushemeji au ukwe, kwani ninaamini CCM bado haijapata mbadala wa kuongoza nchi hii, hivyo tuwaunge mkono watu wenye sifa za kuongoza.”

Kadhalika, alisema chama hicho kimefanya mabadiliko makubwa ikiwamo kuwaondoa viongozi ambao walikuwa wanakiuka maadili.

“Kuna viongozi ambao wao walikuwa wanakopa hawalipi. Kuna  viongozi ambao wao ndio walikuwa wanajihusisha na kangomba, tumewaondoa na tunaendelea kuwapunguza wale ambao wanakiuka maadili.

“Sisi tunashirikiana na vyama vingine duniani, hivyo vinapaswa kuona namna tulivyo nyooka katika maadili,” alisisitiza.

AWAAGA KWA AINA YAKE

Rais Samia ambaye amemaliza ziara yake ya siku nne mkoani Ruvuma, mara baada ya kuhutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika uwanja wa Majimaji, aliamua kutembea huku akiwapungia mkono kisha baadaye kupanda katika gari na kuondoka.

Katika hotuba yake, Rais Samia aliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na serikali mkoa huo kuhakikisha wanapunguza uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali yenye matatizo.

Kuhusu barabara kutoka Songea-Makambako, alisema iko katika mchakato na serikali inafanya kila njia kuikarabati na ile  kutoka Likuyufusi- Mkenda mpakani mwa Msumbiji na Tanzania, itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kilometa 60.

Kwa upande wa elimu, alisema kwa sababu shule ya Rais Samia Suluhu Hassan kuonesha mfano mzuri wa kutumia gesi, ameagiza shule nyingine pamoja na taasisi mbalimbali ziige mfano.

Awali, Mwenyekiti wa UWT, Mary Chatanda, akizungumza katika kilele cha Baraza Kuu UWT, alisema wamejipanga kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo uchaguzi zijazo.

“Sisi tayari tumeshaanza kuunda kamati za ushindi katika uchaguzi mkuu mwakani na ushindi ni lazima mitano tena kwa mwenyekiti wetu,” alisema.

Alisema UWT inakemea tabia ya baadhi ya wanawake wa chama cha upinzani ambao hivi karibuni walimshambulia kwa kumwita muuaji.

“UWT inalaani kitendo cha wanawake hawa kumwita mwenyekiti wetu kuwa ni muuaji wakati wao ndiyo kipindi cha nyuma katika siku ya wanawake duniani walimwalika na kumpatia tuzo kwa kazi nzuri aliyoifanya hali hii haikubaliki na sisi tumechoka kuwavumilia,” alisema Chatanda.

IMEANDALIWA na Paul Mabeja (DODOMA) na Gidion Mwakanosya (RUVUMA)