MAMA wa mtoto mwenye umri wa miaka miwili na miezi mitatu, anasimulia alivyonusurika mtoto wake baada ya kulishwa wali na uji pekee kwa miezi minne mfululizo bila kuchanganya lishe nyingine.
Baada ya hapo alikumbwa na tatizo kisha kupelekwa kwa mganga wa kienyeji kutibiwa hali ikawa mbaya zaidi, mwisho akaponea hospitalini.
Ni baada ya yeye kwenda mjini kutafuta maisha na kumwacha mtoto wake kwa shangazi yake, Maria Kasinje (42), wakati huo akiwa na umri wa mwaka na miezi saba.
Katika Kijiji cha Bubinza, Kata ya Lubugu, wilayani Magu, mkoani Mwanza, mwandishi wa habari hii anakutana na Sundi Charles (20), mama wa mtoto huyo wa kiume ambaye anasimulia kisa mkasa mzima.
Anasema mtoto wake aliacha kunyonya akiwa na mwaka na miezi mitatu na alipofikisha mwaka na miezi saba, alimwacha nyumbani kwa shangazi yake na kwenda Nyamagana kufanya kazi za ndani.
“Kama unavyojua wali ni chakula pendwa katika jamii yetu kwa sababu ya upatikanaji wake. Si wa mara kwa mara, hivyo mtu anapopikiwa huona ameoneshwa upendo wenye thamani kubwa.
“Nilipoondoka kijijini, shangazi alinisimulia kuwa alikuwa akimpikia mtoto wali kila siku na mara moja moja kumlisha uji wa mahindi usiokuwa na lishe ndani yake.
“Baada ya miezi miwili tangu niondoke nyumbani, nilianza kupokea simu kujulishwa mtoto kuugua mara kwa mara, mwili unachemka mara kulegea na kukataa kula. Alikuwa anampikia wali, maarufu kama bokoboko na kumpatia na chai,” anasimulia.
Kutokana na hali hiyo, anasema mtoto alianza kuvimba tumbo na kuwa gumu, hivyo shangazi alimshauri arudi kijijini ili kumpeleka kwa mganga wa kienyeji kwa ajili ya matibabu. Anasema walimpeleka kwa mganga na kukaa kwa wiki akipatia huduma ya tiba bila mafanikio.
“Niliona kabisa ninaelekea kupoteza mtoto kwa sababu hali yake iliendelea kuwa mbaya, hivyo nikaamua kumpeleka hospitalini ambako walibaini tatizo ni lishe na alikutwa na minyoo na upungufu wa damu.
“Huwezi kuamini nilipomwacha mtoto alikuwa na kilo 11 lakini zilishuka hadi kilo nane. Niliamua kukaa na mwanangu na kufuata masharti niliyoelezwa hospitalini kwa kumpatia lishe bora na kamili,” anasimulia.
Anasema kadri alivyokuwa akimhudumia kwa kumbadilishia lishe, mtoto alianza kurejesha katika afya yake. Alisema awali alikuwa hawezi kuongea mpaka wakadhani ni bubu lakini sasa anaongea.
MTAALAM AFUNGUKA
Akizungumza na Nipashe kutoka Hospitali ya Ihayabuyaga, Dk. Mubarak Irunde, anasema tatizo la utapiamlo hujitokeza endapo mtoto akipatiwa chakula cha aina moja.
Anasema mtoto anapopatiwa chakula cha aina moja, huchangia udumavu na kudidimiza maendeleo yake ya ukuaji.
Dk. Irunde anasema mtoto anapofikisha miezi sita ndio kipindi cha kujaribu kumpa vyakula vingine tofauti na maziwa ya mama.
“Mfano hupewa maziwa tofauti na ya mama na uji mwepesi ambapo inapendekezwa kupewa uji wa dona ambapo unaweza kuongoza maziwa na sukari kidogo. Mtoto anatakiwa kupewa makundi yote ya chakula ili kumwezesha kupata virutubisho vyote vinavyotakiwa ili kumsaidia katika ukuaji mzuri na kumwepusha na udumavu,” anasema.
Anasisitiza kwamba udumavu huchangiwa mtoto kutokuendelea na makuzi mazuri ikiwamo ya kiakili kwa sababu hutegemeana na vyakula hasa vyenye protini.
Pia anasema kuna dalili mbalimbali ambazo zinaonesha utapiamlo kwa mtoto zikiwamo kuvimba tumbo, miguu, uso kujaa, nywele kunyonyoka ama kutokuwa na afya, mwili kupauka, kupungua kwa uzito, mtoto kula sana lakini aonyeshi mabadiliko yoyote.
“Wazazi wanapaswa kuwaandalia watoto vyakula vinavyogusa makundi yote, pia ni vyema wakawa na bajeti ya kununua chakula cha mtoto na kuzingatia utaratibu wa kumpima uzito ili kujua maendeleo yake.
“Mtoto anapaswa kula mara tano hadi sita kwa siku unampa chakula kidogokidogo mara moja moja, unampa supu ya nyama, maziwa kwa wingi, dawa za minyoo na kumpima wingi wa damu, itasaidia kuimarisha afya ya mtoto,” anabainisha.
OFISA LISHE ANENA
Ofisa Lishe kutoka Tanzania Early Childhood Education and Care (TECEC), Jackson Yawi, anasema katika makuzi, mtoto anapaswa kupata vyakula ambavyo vinagusa makundi tofauti ili kumsaidia katika ukuaji wake hasa vyenye vitamini A, mfano viazi lishe.
Anasema kadri mtoto anavyozidi kukua, anapaswa kula walau milo minne kwa siku na milo mikuu ni mitatu ikijumuishwa na matunda, juisi asili na maji.
Yawi anasema utumiaji wa aina moja chakula ni tatizo kwa sababu haukidhi mahitaji ya mtoto katika lishe ambaye anapaswa kupata virutubisho vingine.
Anasema kuna madhara mbalimbali ambayo mtoto anaweza kuyapata kwak utumia aina moja ya chakula, ukiwamo utapiamulo ambao unaweza kusababishwa na lishe hafifu au lishe duni ambayo huchangia kuingia katika hali ya ukondefu na udumavu.
Pia alisema hali hiyo huchangia upungufu wa madini chuma na kupungukiwa baadhi virutubisho muhimu ambayo inachangia mtoto kuwa na uelewa mdogo hasa darasani.
“Si lazima mzazi uwe na uwezo lakini unaweza kujali afya yake kulingana na mazingira uliyomo. Mfano unaweza ukawa na unga wa mhogo na mahindi, ukapika uji wako wa mahindi tu wakati wa kupika ukatupia yai moja au ukapika bokoboko unatumia mboga za majani unampa mtoto inasaidia,” anaelimisha.
Yawi anasema katika kutoa elimu lishe amekuwa akifikia zaidi ya wazazi 50 kwa wiki ili kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa lishe kwa mtoto. Anasema tatizo lililoko ni mwitikio wa wazazi wa kiume kutolipa kipaumbele suala la elimu kuhusu lishe.
Agosti 31, mwaka huu, Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, alisema wizara hiyo inaendelea kukamilisha Sera ya Chakula na Lishe ili kukabiliana na utapiamlo na udumavu nchini kwa kujumuisha mapendekezo yaliyotolewa kwenye mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe.
Ripoti ya Lishe ya Watoto iliyotolewa Juni, mwaka huu, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), inabainisha kuwa asilimia 22 ya watoto nchini wanakabiliwa na umaskini wa chakula kwa kiwango kikubwa na asilimia 59 katika kiwango cha kati, hali inayohatarisha ukuaji wao.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 27 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, sawa na watoto milioni 181 wanapata milo isiyozidi miwili kati ya minane inayotambuliwa na shirika hilo.
Kati ya watoto hao, milioni 64 wanaishi kusini mwa Asia na milioni 54 kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania, Uganda, Afrika Kusini, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zikiwamo.
Nchi zingine ni Afghanistan, Bangladesh, China, Ivory Coast, Ethiopia, Ghana, India, Indonesia, Myanmar, Niger, Nigeria, Pakistan, Philippines na Yemen.
Miongoni mwa watoto hao, wanne kati ya watano hulishwa tu maziwa ya mama na au bidhaa za maziwa au chakula chenye wanga, kama vile mchele, mahindi au ngano; chini ya asilimia 10 hulishwa matunda na mboga na chini ya asilimia tano hulishwa mayai, nyama, kuku na samaki.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED