Polisi yaonya watu kutumia mgongo wake kufanya uhalifu

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 10:20 AM Oct 06 2024
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.

JESHI la Polisi limeonya baadhi ya watu kufanya matukio ya uhalifu yakiwamo ya watu kupotea au kutekwa kwa kutumia mgongo wa chombo hicho.

Akizungumza jana mkoani Dar es Salaam katika kongamano la kitaifa dhidi ya matukio ya kupotea na kutekwa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, alisema mara kadhaa jeshi hilo limekuwa likikamata wahalifu wanaojifanya askari polisi au kutoka mamlaka zingine za dola. 

Kongamano hilo limeitishwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na kushirikisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, wanasiasa na Jeshi la Polisi.

Kamanda Muliro alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali kuhusu tukio la mauaji ya kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ali  Kibao, ambaye alikutwa ameuawa baada ya kuchukuliwa kwenye basi na watu waliojitambulisha askari waliokuwa na silaha.

Akifafanua kuhusu matukio ya aina hiyo, Kamanda Muliro alisema mara kadhaa wamekamata watu wanaojifanya askari wa Jeshi la Polisi au kutoka vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

“Kwa hiyo kusema kwamba wale ni polisi kabla ya uchunguzi haujafika mwisho, ninadhani tusijenge utamaduni huo. Tujenge tabia ya kuheshimu mamlaka za kiuchunguzi ili zifanye kazi katika kuitafuta haki. Tunaweza kujikuta tunaumiza watu ambao hawana makosa halafu baadaye tukapata majuto.

“Likitokea tukio ninashauri wanazuoni na wanataaluma wa masuala ya kisheria tujenge tabia ya kuviamini vyombo vya kiuchunguzi, haiwezekani tukaenda kwa mfumo kwamba kila jambo tume.

“Mnakumbukumbu kuna kipindi serikali fulani kila jambo tume, ilikuwa kama miradi ya watu kula fedha tena ikapigiwa kelele, lazima tuamini vyombo vipo kisheria vifanye kazi,” alisema.

Kamanda Muliro alisema endapo litatokea jambo halijakwenda sawa, watumie mifumo ambayo ametumia Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ya watu kuzungumza. Alisema haiwezekani kila chombo kilichoundwa kisheria wakakikataa.

Kuhusu kuwapo chombo huru nje ya polisi, Kamanda Muliro alisema: “Nilitaka nikukumbushe jambo moja la kuheshimu vyombo vyetu kama tabia ya kuheshimu wanasheria wetu kuheshimu majaji wetu.

“Tusirudi kwenye ukoloni. Wapo waliosoma vizuri lazima tuwaheshimu. Mamlaka  hizi zimefanya kazi kubwa sana pamoja na dosari za kiuchunguzi dhidi ya baadhi ya waliopotea au kutekwa. Iko idadi kubwa ya waliotekwa na kupotea wamepatikana. Zaidi ya watu 37 walipotea na wamepatikana kwa sababu tofauti,” alisema.

Kamanda Muliro alitaja baadhi ya sababu za matukio ya aina hiyo katika uchunguzi wao ni kulipiza kisasi, masuala ya hasira au madai ya kudhulumiana, ushirikina na hapo wanaotumia mwamvuli wa Jeshi la Polisi kujitambulisha kama askari.

Kadhalika, alikanusha kuwa si kila aliyepotea au kutekwa ni CHADEMA kama mitazamo ilivyo na kufafanua kwamba baadhi ya watu aliofuatilia katika uchunguzi katika visa kama 37 hawakuwa wa chama hicho bali kutoka vyama mbalimbali.

“Lakini kwenye uchunguzi ukihoji ukienda mbali unakuta si CHADEMA, CCM au ACT -Wazalendo unaweza kukuta ni wa vyama tofauti, lakini amekutwa na kadhia hii. Ndiyo maana ninazo baadhi ya sababu zaidi ya nane ambazo zinasababisha kutokea kwa aina hii ya matukio wakati tunachunguza mambo hayo.

“Baadhi ya masuala ya kiuchunguzi yanatakiwa kabla ya hayajafanyiwa uchunguzi tusiyahukumu kwa sababu unaweza kukuta sababu za matukio yale ni tofauti na namna unavyoelezea,” alisisitiza.

Alipoulizwa kama ameshindwa kukabiliana na matukio hayo mkoani humo, alisema somo la kiuchunguzi liko tofauti hasa wanapofuata misingi ya haki bila kuonea mtu au kubambikiza kesi.

“Ukifanya upelelezi kwa presha unaweza kujikuta unabambikiza kesi mtu au watu kwa ajili ya kuridhisha watu uchunguzi si kama hesabu za kidato cha pili,” alisema.

MWABUKUSI ALONGA

Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, alisema wako hapo kwa sababu jamii yoyote iliyostaarabika na inayoamini misingi ya utu na uadilifu kama inavyoainishwa chini ibara ya 9 ya Katiba. Alisema kunapotokea changamoto hutafuta njia bora na sahihi na kutatua.

“TLS inaamini kunapokuwa na tatizo jambo la kwanza na la msingi ni kukubali kuwapo wa tatizo husika. Ukishatambua na kukubali tatizo unaligeuza kuwa changamoto na kulitafutia majawabu na siyo majibu. Uwapo wa TLS ndio kiungo kizuri kati ya wananchi na seriali yao, kwa mujibu wa sheria kifungu cha 4,” alisema.

Mwabugusi alisema ni lazima wawe na sehemu ya kukutana na kuzungumza kwa sababu ndio mahali kunakotoa fursa ya kuelewa kile mwenzake amefanya na kupitia hapo wanakubaliana waendaje.

“Unapomwona mwenzako amekwenda tofauti unasema wewe si mwenzetu. Kukutana kwa pamoja ni fursa zetu kuzungumza yanayotusibu kwa njia ya staha na katika uhalisia wake na kwa namna ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto hii, huku taifa likibaki imara na salama kwa sababu tuna taifa moja tu,” alisema.

Alisema TLS kupitia wajibu wake kifungu cha 4, wameona wakutane na wadau hao, badala ya wengine kutoa kauli na wengine kukanusha.

“Biblia inasema si mtu mzima atafutaye mganga, bali mgonjwa atamanie kupona. Kama ninakulaumu halafu nikaseme, ninataka kukaa mwenyewe bila wewe kunisikiliza na mimi kusikiliza tutafikia wapi mwafaka?” alihoji.

Baadhi waliochangia katika mkutano huo ni pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Morabvian la Uamsho Tanzania, Emmaus Mwamakula, ambaye, alitoa wito wa kukaa kama baraza la watu wazima kuongea masuala hayo.

“Rais ana uwezo mkubwa kuita viongozi hasa wa dini na wastaafu wakubwa ndani ya nchi hii kujadiliana namna ya kutoka katika uchafu huo,” alisema. 

Naye Katibu Mkuu wa Shura ya Maimam, Shekhe Issa Ponda, alisema mjadala wao ujikite namna ya kuzuia utekaji na mapendekezo yaliyotolewa ni namna gani ya kutunga sheria.

“Hawa watekaji ni watu waliokamilika wana vikisi, wana magari na suala. Kwa lugha nyepesi kuna vikosi vya kuteka watu, lazima tujue asili yake na tunavizuiaje,” alisema.