Polisi yanasa mtandao watuhumiwa wa mauaji

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 09:13 AM Sep 29 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma limekamata genge la watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na matukio manne ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni jijini hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuwataja watuhumiwa hao kuwa ni Paulo Daudi Mwaluko (22), Isack Richard (24), Erest Richard (18) na Silvanus Shotoo (21), wote wakazi wa Mtumba jijini hapa.

Kamnda Katabazi alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika katika tukio la  Julai Mosi, mwaka huu, katika eneo la Mahomanyika, Nzuguni la mauaji ya mabinti wawili ndani ya glosari waliyokuwa wakifanya kazi kisha miili yao kuchomwa moto.

Alisema tukio la pili lilitokea Agosti 28 mwaka huu, eneo la Mbuyuni Kizota ambako aliuawa Michael Richard (36), mke wake na watoto wao watatu waliojeruhiwa na kufungwa katika godoro walilolalia kisha kuchomwa moto ili waungue.

 “Tukio la tatu ni ambalo limetokea Septemba 6, mwaka huu, eneo la Mkonze ambapo mama mmoja na mtoto wake waliuawa, tukio la nne lilitokea Septemba 16 mwaka huu, huko katika Mtaa wa Segu Bwawani Nala ambapo mabinti watatu waliuawa na kuchomwa moto na mama mwenye nyumba kujeruhiwa,” alisema.

Katika tukio la Nala, waliuawa Milcah Robert (12) aliyehitimu darasa la saba Shule ya Msingi Chihoni, Fatuma Mohamed (20), dada wa kazi, Makiwa Abdallah (16) huku Mama Lusajo Mwasonge (40) akijeruhiwa. Tukio la Mkonze Mama Mwamvita Mwakibasi (33) na mtoto wake Salma Ramadhan (13) waliouawa.

 Kamanda Katabazi alisema uchunguzi umebaini kuwa katika matukio yote hayo watuhumiwa walikuwa wakishapiga kwa kitu kizito wanaowakuta katika nyumba walizovamia huwafanyia vitendo vya udhalilishaji na kuwachoma moto ili ionekane ni hitilafu ya umeme imetokea.

“Uchunguzi zaidi unakamilishwa ili hatua zingine za kisheria zifuate, hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao uliofanikisha kukamatwa kwa mtandao huu wa mauaji,” alisema.