JESHI la Polisi limekanusha taarifa za kukamatwa kwa Askofu mstaafu wa Dayosisi ya KKKT Kaskazini Mashariki, Dk. Stephen Munga, ambazo zimeenea katika baadhi ya mitandao ya kijamii kwamba kongozi huyo anashikiliwa na jeshi hilo.
Akizungumza jana na Nipashe, iliyotaka kujua ukweli kuhusu taarifa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Muchunguzi, alisema kiongozi huyo wa dini mstaafu hashikiliwi na jeshi hilo.
Katika taarifa ya Askofu Emmaus Mwamakula, aliyoandika kwenye ukurasa wa kijamii wa Facebook, alidai kwamba aliongea na Askofu Munga akiwa kituo cha polisi kutaka kujua tuhuma zake, lakini hawakuwa na uhakika kwani ilisemekana ni tuhuma za kughushi nyaraka alipokuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Tanga.
Alisema kwamba Askofu Munga, ni miongoni mwa maaskofu watetezi wa haki na kwa sababu ya misimamo yake isiyoyumba, "amelipa gharama kubwa sana na kupata misukosuko mingi na miaka ya hivi karibuni aliwahi kuugua ugonjwa wa ajabu na katika mazingira ya kutatanisha sana, ilibidi akimbizwe Afrika Kusini, ndiko ambako aliponea."
Alisema wanalifuatilia kwa umakini suala hilo na wataujulisha umma kwa kila hali.
Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya KKKT, Dk. Benson Bagonza, pia aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, kuwa "Polisi wameletewa". Andishi la Askofu Bagonza lilikuwa kama ifuatavyo:
POLISI WAMELETEWA
1. Unapopelekwa polisi na mtu ambaye ndiye angekudhamini kama ungekamatwa na polisi kwa kosa lolote - usihangaike kutafuta dhamana.
2. Unapopelekwa kwa mtu ambaye ndiye angeletwa kwako umsaidie; ujue viwango vya ustahimilivu vimeyumba. Aliyepeleka, aliyepelekewa na aliyepelekwa wako msalabani. Hekima itawale - matumizi ya mamlaka, madaraka havina nafasi.
3. Tumezoea kuona Dola ikitumia dini kwa mikakati ya kisiasa. Ukiona dini inatumia Dola katika mikakati yake ujue chumvi imechacha. Dini ikikosa ushawishi ni hatari kuliko sumu na bangi. Muuzeni askofu, ili madeni yalipwe na tukomboe mali zinazouzwa.
4. Kiongozi wa kweli wa dini afurahie kupelekwa Polisi na hata kwa Pilato. Yeye si wa kwanza. Alitangulia Bwana Yesu Polisi na kwa Pilato. Alikutwa na hatia isiyo hatia. Hatia isiyo hatia humwendea aliyepeleka na aliyepelekewa. Yesu alipopelekwa na kuhukumiwa, ulimwengu uliokolewa. Askofu akidhalilishwa, madeni yatalipwa?
5. Jinsi unavyomshughulikia mstaafu yeyote ndivyo unavyowafundisha wasaidizi wako namna ya kukushughulikia utakapostaafu. Polisi msinunue kesi isiyo na bei. Ya sirini yakiletwa hadharani, ya hadharani yataenda sirini.
Nawatetea polisi kwa sababu wameletewa mzigo. Sema tu, mizigo mingine ni kama ya dawa za kulevya. Ukikamatwa nao, unakusumbua wewe.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED