Nesi asimulia walivyompokea Lissu baada ya kupigwa risasi

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 02:20 PM May 19 2024
Tundu Lissu akiwa hospitani.

MUUGUZI aliyemhudumia Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokraasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, baada ya shambulio la risasi, amesimulia walivyompokea, huduma waliyompatia na neno lake la mwisho kabla ya kuzirai.

Akisimulia mkasa huo kupitia video iliyosambaa mtandaoni baada ya Lissu kukutana na muuguzi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Veronica, amesema wakati anafikishwa hospitalini hapo, yeye na wenzake akiwamo daktari aliyemtaja kwa jina la  Bundala, walikuwa Idara ya Wagonjwa wa Nje (OPD).

“Tulikupokea OPD ukiwa umeloa damu, huyu baba alikuwa ameloa damu kutoka mwilini kwako, tukakuingiza chumba cha dharura. Ninataka nikupe sentensi yako ya mwisho uliyoongea na mimi. Huwezi ukanikumbuka. Kiukweli mheshimiwa uliumia.

“Sasa tulikuwa tukishika mkono unaning’inia. Tukikamata huku unaning’inia, tukishika mguu unaning’inia. Tukawa tunaendelea kukuhudumia ili damu isiendelee kutoka lakini ikawa inatoka.

“Ikabidi tuchukue toroli. Nilikuwa  mimi na nesi anayeitwa Elizabert, Daktari Bundala, tukakimbia mpaka chumba cha upasuaji. Kufika bahati mbaya tukakuta madaktari wamemaliza upasuaji wametawanyika,” amesimulia.

Muuguzi huyo amesema kutokana na hali hiyo, ilibidi yeye na mwenzake waendelee kumhudumia wakati madaktari wakitafutwa huku daktari Samwel akiwa wa kwanza kuingia wakimsubiri mwingine.

“Tukikuangalia tunaona unaendelea kutokwa damu ndipo nilipochana bukta yako,” anasimulia nesi huyo huku Lissu akimtania alikuwa amevaa bukta au suruali na kumweleza kuwa suruali waliitupa OPD na anaongea hayo kwa kuwa anaona sasa anapumua.

“Huyu baba aliumia. Sisi hatukuwa wasemaji lakini mimi ndiye muuguzi niliyempokea na hata dereva ndiye niliyemkabidhi zile nguo, Mheshimiwa (Freeman) Mbowe (akiwa) pembeni. Nilifika  na nguo zake nikitokea chumba cha upasuaji.

“Ila kabla sijatoka (chumba cha upasuaji) ulianza kutoka jasho, huku daktari anakutundikia dripu mkono mwingine, ulichotamka ulisema, “Please Doctor do something for me” ukalegea.

“Nilitoka na damu, mtu wa maabara alikimbia, kupima ulikuwa na damu tatu. Ninaongea ukweli mbele za Mwenyezi Mungu, huyu Mheshimiwa damu ilikuwa tatu. Kilichoendelea  ninafikiri unajua,” alimweleza Lissu huku akijibu, atajuaje.

Amesema akiwa muuguzi, aliishia hapo na kukabidhi nguo na kwenda kuchukua damu wakati madaktari wakiendelea na upasuaji wake.

“Ulichotamka ni ‘Doctor do something for me’, uliongea Kiingereza hukuongea Kinyaturu,” alimsimulia, huku Lissu akimpa pole akimweleza wanaona vitu vya ajabu.

“Mimi sikuviona vyote hivyo,” alisema Lissu huku muuguzi huyo akimtaka amshukuru Mungu wake mpaka sasa yupo.

Alimweleza kuwa wanapofanya kazi alafu mgonjwa akapona wanapata baraka na kushukuru na kwa hali yake, hakutegemea siku moja angekutana naye.

Baada ya maelezo hayo, Lissu alihoji kwa nini wanajificha wakati madaktari wake wote na manesi waliomtibu Nairobi, Kenya anawafahamu lakini hapa huyo ndiyo wa kwanza anakutana naye.

Muuguzi huyo alimfafanulia kwamba taratibu za Tanzania ni tofauti ndiyo maana hata siku ya tukio walipokuwa wakipiga picha, kiongozi wao aliwataka wakae pembeni wasionekane.

“Unajua pale hospitalini palijaa watu, tukawa tunaogopa usalama wako. Hakuna  mtu aliyeruhusiwa kuingia chumba cha upasuaji bila kitambulisho na tulifunga milango yote, sisi wa mapokezi tukarudi kuendelea na kazi zetu, huku tukipata taarifa unavyoendelea mpaka ulipokwenda Nairobi.

“Ila chupa za damu baba ulikula. Madaktari waliokuhudumia walikuwa ni Dk. Samwel na Dk. Ibenus ndiyo waliokuwapo pale,” amesema.

Muuguzi huyo alimweleza Lisu kuwa  alipoteza fahamu pale alipokuwa akimtundikia dripu na kutamka sentensi yake ya mwisho. Muuguzi huyo alisema kwa sasa ana miaka miwili hayupo kazini, aliondoka Aprili, 2020.

MJADALA UNUNUZI GARI

Katika hatua nyingine, siku moja baada ya Jeshi la Polisi kumkabidhi gari lake Lissu, mjadala umeibuka mtandaoni huku baadhi wakitaka kumchangia fedha ili kununua jipya, wengine wakiona hoja hiyo ni mzaha kwao.

Manaharakati Maria Sarungi, katika ukurasa wake wa Instagram baada ya Lissu kukabidhiwa gari lake lililokaa polisi kwa miaka saba, ameibua hoja ya kumchangia fedha ili anunue gari jipya.

Sarungi aliweka tangazo lenye maelezo yanayosomweka: “Tumchangie Tundu Lissu anunue gari jipya,” huku akiweka namba za kupokelea na  akaunti.

Aliwataka wale wanaotaka gari la Lissu liwekwe kumbukumbu wazingatie kwamba hana gari kwa sasa, anakodi kwa fedha nyingi na hawezi kumudu. Pia alisema Lissu anahitaji gari ili kuzunguka nchi nzima kutoa elimu.

Baadhi walipokea hoja hiyo na kupendekeza anunuliwe gari aina ya Land Cruiser 300 (LC300) huku wengine wakiona ni kichekesho kumnunulia mtu mwenye fedha gari wakati familia zao hazina chakula.

Wakati mjadala huo ukiwagawa wachangiaji, mwingine amependekeza gari alilokabidhiwa na polisi lisiguswe liachwe lilivyo kwa kuwa litaacha alama kubwa na kueleza kuwa ifikapo Mei 30, atakuwa na gari lingine.

Mchangiaji anayejiita bin.rama, alichangia kwa kuweka emoji ya kucheka na kuandika: “Mbona uhuni wa macho macho unatuletea wewe bi mkubwa. Ok (sawa) toka lini magari wanayozunguka nayo CHADEMA wanakodisha? Maruzuku wanayopewa unaweza kuniambia kazi yake nini?”

Mchangiaji mwingine anayejiita Salum8082, aliandika kuwa, “Yaani mimi nitoe pesa zangu nimchangie mtu akanunue gari mtu anayemiliki zaidi ya nyumba moja si auze moja anunue gari?”

Thereataita_kuku_tamu, alichangia kwa kueleza kuwa iweje aache kumchangia mama yake kijijini anunue unga, akamchangie tajiri anunue gari.

“Hata kama analo lingine, lakini kuonyesha umoja wetu wa watu wanaompenda haki na kuonyesha wanao tudhulumu haki kwamba, tuko imara katika umoja wetu.

“Lazima tumnunulie Mheshimiwa Lissu gari jipya zuri zaidi tena lenye uwezo wa kuzuia hata risasi na mabomu. Nashauri wachangishaji waongezeke watu wote wenye wafuasi wengi waweke bango hilo la michango,” alishauri Muyigw.

Mhagule_aliandika kuwa atatoa chochote alicho nacho kwa kuwa Lissu analindwa na Mungu.