Mradi bil. 104/- kupaisha sekta ya madini

By Ashton Balaigwa , Nipashe Jumapili
Published at 07:58 AM Jun 02 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

SERIKALI inakusudia kutekeleza mradi mkubwa wenye thamani ya Sh. bilioni 104 utakaotoa umeme wa uhakika kwa wawekezaji wa migodi ya madini katika wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.

Aidha, serikali inatarajia kutangaza wakati wowote wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero kuwa ni mkoa wa shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutokana na umuhimu maeneo hayo katika kuzalisha mazao mbalimbali yanayosaidia kukuza uchumi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alisema hayo mjini hapa wakati akizindua mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme wa uhakika kwa wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga.

Kituo hicho kimejengwa na serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU)  kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya  (EDF) kwa gharama ya Sh. bilioni 24.59 ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali za kuondoa umasikini katika kuendeleza kilimo.

Naibu Waziri Mkuu alisema Ulanga ni moja ya wilaya zilizobarikiwa kuwa na madini ya aina tofauti yakiwamo ya Kinywe, vito (spinal), hivyo wawekezaji wengi wamekuwa wakijitokeza kuwekeza lakini changamoto kubwa imekuwa umeme wa uhakika.

“Tunataka kujenga mradi mkubwa wa zaidi ya Sh, bilioni 104 ambao utakuwa unajitegemea kwa kupeleka umeme wa uhakika katika migodi yetu ili kuvutia wawekezaji kutoka nje na tunafanya hivi kwa uzito mkubwa,” alisema.

Kuhusu manufaa ya mradi huo, Dk. Biteko alisema utasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi ambazo zilikuwa na tatizo la a kukatika kwa umeme zaidi ya saa nane kwa siku. Alisema baada ya mradi huo kukamilika, umeme unakatika kwa dakika 46 pale yanapofanyika matengenezo.

Alisema kukamilika kwa mradi huo pia kutawezesha sehemu za biashara na viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo 54 kupata umeme wa uhakika na kufanya ukusanyaji wa mapato kwa TENESCO kuongezeka.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu, alisema wameamua kujenga kituo cha kupoza umeme Ifakara kutokana na wilaya hizo kuzalisha kwa wingi mpunga pamoja na miwa ambayo husaidia kukuza uchumi wa nchi,

Alisema kutokana na umuhimu wake kwa wilaya hizo , tayari vijiji 110 vilivyoko eneo la mradi vimeshapatiwa umeme na vilivyobaki 180, baada ya miaka miwili navyo vitakuwa na umeme.

Naye Balozi EU nchini, Christine Glau, alisema umoja huo utaendelea kuisaidia serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi yake mbalimbali yakuondokana na umasikini.

Alisema kituo hicho ni miongoni mwa vituo 14 ambavyo wanatarajia kuvijenga hapa nchini ambavyo vitakuwa na thamani ya Sh. bilioni 600.

Balozi huyo alisema kuwapo kwa umeme wa uhakika sasa utasaidia wakulima wa mpunga kuuza mchele badala ya kuuza mpunga kwa bei ya chini.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, alisema wilaya hizo tatu za Kilombero, Ulanga na Malinyi kwa muda mrefu zilikuwa zikikabiliwa na changamoto ya umeme licha ya kuwa kinara wa uzalishaji wa mpunga na miwa.

Alisema asilimia 70 ya sukari inayozalishawa nchini inatoka mkoa wa Morogoro ambao una viwanda vinne vya kuzalisha sukari  pamoja na kuzalisha mpunga.