Miili iliyoopolewa ajali ya boti yafikia tisa

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 08:16 AM Sep 29 2024
Miili iliyoopolewa ajali  ya boti yafikia tisa
Picha:Mtandao
Miili iliyoopolewa ajali ya boti yafikia tisa

MIILI ya watu saba imeopolewa katika Ziwa Victoria na kufanya idadi kufikia tisa baada ya ajali ya boti ya mizigo ya MV. Sea Falcon.

Boti hiyo ilikuwa na zaidi ya abiria 30 ikitokea Kirumba mkoani Mwanza kwenda kisiwani Goziba, kilichoko mkoani Kagera.

Ajali hiyo ya boti lenye usajili namba MTZ 012212 ilitokea juzi Septemba 25 mwaka huu, saa 12:00 asubuhi katika Ziwa Victoria kilometa mbili kutoka nchi kavu ya mwalo wa Bwiru ulioko wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.

Akizungumza jana wakati wa uopoaji wa miili hiyo, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Ilemela ambaye pia ni Kaimu Kamanda Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Msaidizi (ASF)  Deusidedith Ruta, alisema mwili wa pili uliopolewa juzi majira ya jioni.

“Leo (jana) tumeopoa miili saba na kufanya idadi kufikia tisa na miili yote ni ya jinsia ya kiume. Kati ya miili hii, miwili pekee ndiyo imetambuliwa na ndugu,” alisema Ruta.

Alisema miili yote imepelekwa katika Hospitali ya Rufani Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure) na kuwa shughuli ya utafutaji  katika eneo la tukio bado inaendelea kutokana na kutokuwapo kwa idadi rasmi ya watu waliopanda boti hiyo.

Alisema baadhi ya miili ilipatikana katika eneo ilikozama boti hiyo, huku mingine ikipatikana katika maeneo mbalimbali ya fukwe za Ziwa Victoria.

“Kutokana na hali hiyo, niwaombe viongozi wa wavuvi pamoja na wavuvi pindi watakapoona miili ikielea wasisite kutoa taarifa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuifikisha katika maeneo rasmi.

“Niwatake ndugu wanaohisi kuwa walikuwa na ndugu zao katika boti hili kuhakikisha wanafika katika hospitaliya Sekou Toure ili kutambua ndugu zao,” alisema Ruta.

Akizungumza katika eneo la tukio, shuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni mmiliki wa eneo la mwalo walipokuwa wakipokewa majeruhi hao pamoja na miili iliyoopolewa, Joseph Masole, alisema mtu wa kwanza kuwapatia taarifa hiyo alikuwa miongoni mwa manusura wa ajali hiyo.

 “Alifika akasema tupo watu kama 60, tunahitaji msaada nikatuma mitumbwi ikaenda kuokoa watu na wakati huo tukiendelea na kuomba msaada kutoka vyombo vya ulinzi na usalama ambako gari za wagonjwa zililetwa kwa ajili ya kuwapokea wote waliokuwa wakiokolewa,” alisema Masole.

Kamanda wa Polisi Mkoa Mkoa wa Mwanza,  Naibu Kamishna (DCP) Wilbroad Mutafungwa, alithibitisha kuwakamata watu watatu akiwamo mmiliki wa boti hiyo, Amon Lutabanzibwa, kutokana na kutumia boti hiyo kubeba abiria bila kuwa na kibali cha kufanya kazi hiyo kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

“Miili minne tayari imetambulika na kukabidhiwa kwa ndugu ambako serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imetoa majeneza, Sh. 100,000 kwa kila familia pamoja na kugharamia usafirishaji wa miili,” alisema DCP Mutafungwa.

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti kutoka TASAC, Leticia Mutaki, alisema leseni ya boti hiyo inataka kibebe watu wasiozidi watano, lakini wenyewe walibeba zaidi ya 30.

Kutoka na tukio hilo, Mutaki aliwataka wamiliki pamoja na wasafirishaji wa vyombo vya majini kuzingatia masharti ya leseni wanazopewa na matakwa ya leseni hizo.

“Leseni zimebainisha kabisa kwamba wewe kanuni yako ya kubeba mizigo ni kiasi kadhaa na kama ni abiria ni abiria kadhaa na kwa boti hii iliyokuwa na urefu wa mita 17 kiwango chake ilikuwa ni watu wasiozidi watano,” alisema.