NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Salim Mwalimu Juma, ametuma salamu kwa wanasiasa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu ujao wa Zanzibar atatoka chama chake kutokana na anavyoendelea kujipanga.
Alisema kuporomoka kwa kutopendwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CHADEMA ina uhakika wa kushinda urais Zanzibar kutokana na ilivyojipanga kuongeza idadi ya wanachama na pamoja na kuungwa mkono na CCM na ACT -Wazalendo hasa kisiwani Pemba.
Akizungumza na wajumbe wa mabaraza ya uongozi wa CHADEMA Kanda ya Pemba kwenye ukumbi wa Kibirinzi mjini Chakechake, alisema katika uchaguzi mkuu ujao, chama chake kimedhamiria kuingia kikiwa na uhakika wa kushinda kwa kuwa wameshasoma uchaguzi uliopita.
“Katika chaguzi zilizopita tulikuwa hatuingii tunakaa mlangoni tu tunachungulia ila mara hii tutaingia wote kifua mbele na kwa kujiamini,” alisema.
Alisema miaka yote CHADEMA ilikuwa ikikaa mlangoni na kuchungulia kujua harakati na mbinu zinazotumiwa na CCM na ACT Wazalendo na sasa iko imara kukabiliana na uchaguzi ujao.
Salum aliwasihi wana CHADEMA kushikamana kujenga umoja na kuachana na utegemeo wa aina yoyote wakati huu ambao wananchi wameleta matumaini ya kujiunga kwa wingi katika chama hicho.
Alisema tayari katika uchaguzi unaoendelea ndani ya chama, wamekwisha kufanya uchaguzi kwenye matawi yote ya Pemba na jambo linalotia matumaini ni kuwa hivi sasa kuna baadhi ya matawi yana zaidi ya wanachama 80 wakati ili kuunda tawi wanahitajika wanachama 50 tu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, alisema wanachama wengi wa vyama vya siasa, hujenga makundi wakati wa uchaguzi wa ndani ya vyama vyao na uongozi unaposhindwa kurekebisha huwa sababu ya chama kusambaratika na kukosa ushindani wakati wa uchaguzi mkuu.
Alisema majungu, fitna na mgawanyiko utakaojitokeza kwa njia yoyote haukubaliki na unafaa kupigwa vita usije kukigawa chama wakati huu ambao kimekwisha kukubaliwa na wananchi wengi wanajiunga.
Said alisema inavyoonesha sasa, CCM, ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF) vinakosa wafuasi na kupungua umaarufu lakini CHADEMA inazidi kupata umaarufu kwa kasi, hivyo hawana budi kujizatiti na kuzidi kujipanga ili kufanikisha malengo yao ya kuchukua dola.
Aliwataka wana CHADEMA kuona fursa zilizoko kwa kuwa chama kikishachukua dola, kina nafasi nyingi za uteuzi kiasi kuwa watalazimika kuchukua watu nje ya chama kama watu hawatazingatia na kujiunga kwa wingi ili kukimbilia fursa hizo ambazo zinakuja.
Pia aliwataka wana Chadema kufanya kazi kwa kuwa hakuna sababu ya kushindwa katika uchaguzi wowote unaokuja.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED