Ado: Shida ya Maji Kanda ya Ziwa ni ishara ya serikali kupuuza wananchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 11:58 AM Sep 29 2024
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu.
Picha:Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu.

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu ametupia lawama serikali kwa kushindwa kuwahakikishia upatikanaji wa maji wananchi wa kanda ya ziwa licha ya kanda hiyo kuzungukwa na Ziwa Victoria.

Ziwa Victoria ni ziwa lapili kwa ukubwa lenye majitamu duniani ambapo limezunguka nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Tanzania, Kenya, Uganda.

Sehemu kubwa ya Maji ya Ziwa Victoria ipo Tanzania ambapo ni 49%, Uganda 43% na Kenya 6%.

Kiongozi huyo anasema, licha ya hayo bado wananchi wa Kanda ya Ziwa wanalalamika shida ya maji, wananyang'anyana maji na mifugo kwenye madimbwi, mito na visima.

Katika hotuba yake Ado amesema "ni aibu kwa serikali ya CCM, watu wa kanda ya ziwa, wanaoishi kandokando ya ziwa Victoria hawana uhakika wa maji, ni aibu sana. Hiki ni kiashiria kwamba Wananchi wa Buchosa mmepuuzwa."

Ado ameyasema hayo alipokua anahutubia wananchi wa Buchosa Mkoani Mwanza Sept 28, 2024. Akiwa kwenye mwendelezo wa Ziara yake kanda ya ziwa ikijumuisha mikoa ya Simiyu, Mara, Mwanza, Geita na Kagera.