Ukraine yaishambulia Urusi, yajeruhi watu 17

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:17 PM May 12 2024
Jengo la makaazi katika mji wa Belgorod limeharibiwa katika shambulizi la kombora linalodaiwa kurushwa na Ukraine.
Picha: STRINGER/AFP
Jengo la makaazi katika mji wa Belgorod limeharibiwa katika shambulizi la kombora linalodaiwa kurushwa na Ukraine.

JENGO moja limeporomoka katika mji wa mpakani wa Urusi, Belgorod baada ya shambulizi la Ukraine, na kusababisha watu 17 kujeruhiwa. waziri wa afya wa Urusi Mikhail Murashko amethibitisha.

Wizara ya ulinzi nchini Urusi, imesema kuwa kombora la Ukraine aina ya Tochka-U, lililenga eneo la makazi mjini humo baada ya kudunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga.

Murashko amenukuliwa na kituo cha habari cha serikali RIA Novosti akisema kwamba majeruhi hao 17 wamepelekwa kwenye vituo vya afya.

Wizara ya kukabiliana na hali za dharura imesema watu 12, wanaowajumuisha watoto wawili, wameokolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo hilo.

Wizara hiyo pia imeonya kuwa idadi ya majeruhi inaweza kuongezeka kwa sababu sehemu ya paa la jengo hilo imeporomoka wakati maafisa wa uokoaji walipokuwa wakiwatafuta manusura.

Gavana wa Belgorod Viacheslav Gladkov amelaani mashambulizi hayo ya jeshi la Ukraine.

DW