WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, ameagiza taasisi zote za umma kuzingatia matakwa ya sheria ya ununuzi wa umma na zinazokaidi zichukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Dk. Nchemba aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya mwaka ya utendaji wa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Alisema sheria imeweka kosa la jinai kwa mtu ambaye kwa makusudi ataamua kufanya ununuzi nje ya mfumo wa kieletroniki akibainika na kuthibitika, atapatiwa adhabu ikiwamo kifungo cha miaka mitatu jela.
“Nimesikia kuwa zipo baadhi ya taasisi nunuzi bado zinasitasita kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Umma wa Kieletroniki Tanzania (NeST), ingawa zimewezeshwa kuutumia.
“Nazielekeza taasisi zote za umma kuzingatia matakwa ya sheria ya ununuzi wa umma na kutumia mfumo wa NeST ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha tunapata thamani halisi ya fedha,” alisema.
Dk. Nchemba alisema endapo watakuwa na changamoto yoyote wanapaswa kuwasiliana na PPRA ili wapate maelekezo na idhini ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
“Haiwezekani taasisi imepatiwa elimu ya kutumia mfumo huo alafu hawatumii, jambo hilo halipo sawa taasisi zinazokwamisha wasione aibu kuwachukulia hatua.
“Wananchi tunawataka watumie EFD (mashine za risiti za kielektroniki) halafu taasisi za umma hazitaki kutumia zabuni hizo, taasisi ambazo zinakiuka taratibu za ununuzi wanatakiwa kutangazwa na kufahamika atakayefanya manunuzi nje ya mfumo sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Dk. Nchemba alisema ni marufuku kuagizwa kwa thamani nje ya nchi na yoyote anayehitaji aagize kwa ajili ya nyumbani kwake na sio kwa matumizi ya serikali.
“Ni muhimu kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini mtu anaagiza mawe nje ya nchi ama nondo wakati zinazalishwa hapa nchini huko ni kuongeza gharama. Kama nondo unazozitaka hazipatikani, ingia makubaliano na kiwanda kikutengenezee ukubwa unaoutaka. Tuache mazoea ya kuagiza malighafi nje ya nchi wakati zinapatikana nchini,” aliagiza.
Alisema mfumo huo umesaidia kuboresha mifumo ya udhibiti wa ndani wa taasisi nunuzi na hivyo kuendana na tamko la la Rais Samia Suluhu Hassan, kuitaka Wizara ya Fedha kudhibiti matumizi ya fedha za serikali hasa katika utekelezaji wa miradi.
Alisema bado wana kazi kubwa ya kujenga uwezo na kuhamasisha jamii kuanza na kuendelea kutumia mfumo huo.
Alisema mtokeo chanya ya mfumo huo ni pale mwananchi wa kawaida watakapoweza kupata huduma na bidhaa kwa bei nafuu kulingana na thamani ya fedha.
“Ni muhimu, Bodi ya Wakurugenzi sasa ikaweka mkakati mzuri ili kuhakikisha tunakamilisha ujenzi wa mfumo wa NeST katika moduli mbili zilizosalia kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2024/25,” alisema.
Alisema pia, kuendelea kutoa usaidizi kwa watumiaji wa mfumo ili wizara na nchi iweze kupata faida ya matumizi ya mfumo wa kidigitali na hivyo kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dk. Leonada Mwagike, alisema licha ya mafanikio ambayo wameyapata, ziko changamoto zikiwamo baadhi ya taasisi nunuzi kutotumia mfumo wa kieletroniki katika michakato ya ununuzi.
Alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, taasisi za ununuzi zilipanga kuwa na zabuni 99,671, lakini ni zabuni 53,886 ndizo zilizotangazwa kupitia mfumo wa NeST.
Alitaja changamoto nyingine ni baadhi ya taasisi nunuzi kutokutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalum, yaani wanawake, wazee, vijana na watu wenye mahitaji maalum.
Mwagike alisema mamlaka itachukua hatua kwa kuzishauri hatua za kinidhamu kwa wale wanaokiuka matakwa ya sheria kwa mamlaka husika.
Alisema wameokoa jumla ya Sh. bilioni 14.94 kupitia ukaguzi na Sh. trilioni 2.7 kupitia ufuatiliaji.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED